Chuki dhidi ya Waislamu yaongezeka Australia baada ya shambulio la Bondi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135050-chuki_dhidi_ya_waislamu_yaongezeka_australia_baada_ya_shambulio_la_bondi
Afisa mmoja wa Australia ametoa tahadhari kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu tangu kujiri shambulio la Bondi mwezi uliopita, ambalo lililenga jamii ya Wayahudi wa nchi hiyo katika tamasha la Hanukkah.
(last modified 2026-02-02T06:45:47+00:00 )
Jan 03, 2026 06:01 UTC
  • Chuki dhidi ya Waislamu yaongezeka Australia  baada ya shambulio la Bondi

Afisa mmoja wa Australia ametoa tahadhari kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu tangu kujiri shambulio la Bondi mwezi uliopita, ambalo lililenga jamii ya Wayahudi wa nchi hiyo katika tamasha la Hanukkah.

Aftab Malik, Mjumbe Maalum wa Australia wa Kupambana na Chuki Dhidi ya Uislamu ameonya kwamba, vitendo vya chuki dhidi ya raia Waislamu wa Australia, hasa wanawake, vimeongezeka tangu lilipojiri shambulio katika Ufukwe wa Bondi.

Mnamo Desemba 14, watu wawili wenye silaha, baba na mwana, mmoja kutoka India, mwingine raia wa Australia, wenye uhusiano na kundi la kigaidi lenye misimamo mikali, waliwaua watu 15 katika shambulio hilo la kigaidi katika jiji la Sydney, Australia.

Mjumbe Maalum wa Kupambana na 'Islamophobia' nchini Australia amesema katika makala iliyochapishwa na gazeti la The Guardian jana Ijumaa kwamba, tangu shambulio kujiri la Bondi, baadhi ya Waaustralia wanashindwa kutofautisha kati ya Waislamu wa kawaida na magaidi wanaohusishwa na kundi la kigaidi la Daesh (ambalo pia linajulikana kama ISIS au ISIL).

Malik amesema wanawake Waislamu wameripoti kutemewa mate, kudhalilishwa, kushambuliwa na kutishiwa katika kipindi cha wiki mbili tangu kujiri shambulio hilo. Kabla ya hapo, makaburi ya Waislamu nchini Australia yalinajisiwa kwa vichwa vya nguruwe vilivyokatwa kufuatia hujuma hiyo ya mjini Sydney.

Chuki dhidi ya Waislamu zimeongezeka nchini humo katika hali ambayo, ni raia Mwislamu, Ahmed Al Ahmed, aliyehatarisha maisha yake kwa kumvamia na kumpokonya bunduki mmoja wa wahusika wa shambulio hilo lililotokea kwenye Ufukwe wa Bondi na kusababisha vifo vya watu 15.

Mjumbe Maalum wa Australia wa Kupambana na Chuki Dhidi ya Uislamu ameongeza kuwa, wanaharakati hao wanataka jamii iwena mgawanyiko, ili kumgombanisha jirani na jirani yake, na muumini dhidi ya mwenzake, na kuwalazimisha watu kujenga kuta baina yao.