Mmarekani aliyemuua mtoto wa Kipalestina afariki dunia gerezani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128876-mmarekani_aliyemuua_mtoto_wa_kipalestina_afariki_dunia_gerezani
Mwenye nyumba huko Illinois aliyepatikana na hatia ya kumuua mtoto wa mpangaji wake Mmarekani mwenye asili ya Palestina amefariki dunia akiwa kizuizini.
(last modified 2025-07-29T02:41:17+00:00 )
Jul 29, 2025 02:41 UTC
  • Mmarekani aliyemuua mtoto wa Kipalestina afariki dunia gerezani

Mwenye nyumba huko Illinois aliyepatikana na hatia ya kumuua mtoto wa mpangaji wake Mmarekani mwenye asili ya Palestina amefariki dunia akiwa kizuizini.

Joseph Czuba alihukumiwa kifungo cha miaka 53 jela mwezi Mei kwa mauaji ya Wadea al-Fayoume pamoja na kumjeruhi vibaya na kujaribu kumuua mamake, Hanaan Shaheen, mnamo 2023.

Polisi wanasema kuwa mwenye nyumba huyo aliwashambulia wawili hao kwa sababu ya imani yao ya Kiislamu muda mfupi baada ya kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Sheriff ya Will County, Joseph Czuba aliyekuwa na chuki na Waislamu alikufa katika Kituo cha Marekebisho cha Illinois, siku ya Alhamisi,

Czuba alikuwa ametumikia chini ya miezi mitatu ya kifungo chake cha miongo kadhaa alipofariki dunia kwa sababu ambayo bado haijajulikana akiwa na umri wa miaka 73.

Familia iliyoathirika ilikuwa inakodi vyumba takriban maili 40 (64km) kutoka Chicago, wakati shambulio hilo lilipotokea. Polisi wanasema Czuba alimdunga kisu al-Fayoume (6) mara 26. Mtoto huyo baadaye alifariki dunia akiwa hospitalini.

Czuba alipatikana na hatia ya makosa mawili ya uhalifu wa chuki, kosa moja la mauaji ya daraja la kwanza, moja la kujaribu kuua na mawili ya unyanyasaji mbaya.

Mama wa mtoto huyo alitoa ushahidi mahakamani kwamba Czuba pia alimshambulia kwa kisu kabla ya kwenda kwa mwanawe, akimwambia "wewe, kama Muislamu, lazima ufe", Reuters iliripoti.

Mama huyo hakuhudhuria mazishi ya mwanawe kwani alikuwa akipata matibabu hospitalini kutokana na majeraha aliyoyapata katika shambulio hilo.