Utafiti: UK inaendelea kusakamwa na uchochole
Umaskini nchini Uingereza umezidi kuwa mbaya, huku idadi kubwa ya watu wakiishi katika hali ngumu wasiweze kumudu mahitaji yao ya msingi, hayo ni kwa mujibu utafiti uliofanywa na shirika moja la kutoa misaada.
Wakfu wa Joseph Rowntree umesema karibu watu milioni saba nchini Uingereza wanaishi katika ukata na hali ngumu kupindukia, kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Zaidi ya mtu mmoja kati ya watano nchini Uingereza - takriban milioni 14.2 - walikuwa wakiishi katika umaskini mwaka 2023/24, mwaka wa mwisho wa serikali ya mwisho ya Conservative, na mwaka wa hivi karibuni ambapo takwimu rasmi zinapatikana, Wakfu wa Joseph Rowntree (JRF) umesema katika ripoti yake mpya.
Kati yao, utafiti huo umesema, karibu asilimia 50, au watu milioni 6.8, walikuwa wakipitia shida "nzito sana", idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Utafiti huo umefichua kuwa, watoto, wapangaji, walemavu, na wale walio katika kazi 'zisizo salama' walikuwa miongoni mwa makundi yaliyoathiriwa zaidi.
Karibu watoto milioni 4.5 waliishi katika umaskini mwaka 2023/24, 600,000 zaidi kuliko wakati wa tandavu ya Corona, na kuashiria mwaka wa tatu mfululizo wa ongezeko hilo. Viwango vilikuwa vya juu zaidi katika familia zenye idadi kubwa ya watu, ambapo 44% ya watoto waliathiriwa.
Kadiri uchumi wa Uingereza unavyozidi kulegea na kuporomoka, takribani robo ya wazazi wenye ajira nao wanalazimika kutafuta msaada wa chakula cha bure kutoka mashirika ya hisani. Kwa mujibu wa taasisi ya ‘The Felix Project’, kati ya kila wazazi wanne wenye kazi, mmoja huenda mara kwa mara, kila wiki moja au mbili, katika mashirika ya hisani kwa ajili ya kupokea msaada.