Iran ilivyofanikiwa kuvunja mtandao wa mawasiliano ya kigaidi kwa kukata intaneti
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135992-iran_ilivyofanikiwa_kuvunja_mtandao_wa_mawasiliano_ya_kigaidi_kwa_kukata_intaneti
Iran ilifanikiwa kuvuruga na hatimaye kuvunja mtandao wa mawasiliano wa makundi ya kigaidi na washirika wao wa nje kwa hatua ya kukata intaneti wakati wa machafuko ya Januari 2026.
(last modified 2026-01-28T08:00:48+00:00 )
Jan 28, 2026 08:00 UTC
  • Iran ilivyofanikiwa kuvunja mtandao wa mawasiliano ya kigaidi kwa kukata intaneti

Iran ilifanikiwa kuvuruga na hatimaye kuvunja mtandao wa mawasiliano wa makundi ya kigaidi na washirika wao wa nje kwa hatua ya kukata intaneti wakati wa machafuko ya Januari 2026.

Kwa mujibu wa taarifa ya Pars Today, uzoefu wa Iran katika kukabiliana na machafuko ya ndani, pamoja na mifano kutoka nchi nyingine, unaonyesha kuwa udhibiti wa muda wa intaneti katika nyakati nyeti ni hatua ya lazima, yenye uwajibikaji na ya kinga kwa ajili ya kudhibiti ugaidi wa kidijitali na kukata mawasiliano yao na serikali au vyombo vya kijasusi vya kigeni.

Kukata au kupunguza intaneti wakati wa hatari kubwa za kiusalama, uasi wa kutumia silaha au mashambulizi ya kigaidi ni jambo lenye historia ndefu duniani. Mataifa mbalimbali, ikiwemo baadhi ya nchi za Magharibi, yamewahi kutumia mbinu hii kama kifaa cha dharura cha kulinda utulivu wa ndani na usalama wa taifa.

Katika muktadha huu, hatua ya Iran ya kukata intaneti wakati wa machafuko ya Januari 2026  haikuwa tu uamuzi wa kiufundi, bali sehemu ya mkakati mpana wa kiusalama uliolenga kuvuruga mitandao ya kisiri ya wapinzani wa serikali na makundi yenye silaha yaliyokuwa yakitumia majukwaa ya mawasiliano mtandaoni kupanga operesheni, kupokea maelekezo na kuhamisha taarifa kwenda nje ya nchi.

Uchambuzi wa mwenendo wa matukio unaonyesha kuwa kukatwa kwa intaneti katika kipindi hicho hakukuwa jibu la haraka kwa maandamano pekee, bali ilikuwa hatua ya kimkakati iliyolenga kukata mishipa ya mawasiliano ya mitandao ambayo shughuli zake zilikuwa zimevuka kiwango cha vurugu za mitaani na kuingia katika eneo la operesheni za kiusalama zilizo na uratibu wa nje.

Wakati wa machafuko ya Januari 2026, ripoti za kiusalama zilionyesha kuwa sehemu kubwa ya uratibu wa operesheni ulifanyika kupitia ujumbe uliosimbwa, majukwaa ya kigeni na njia za mawasiliano ambazo usimamizi wake ulikuwa nje ya nchi.

Njia hizi hazikubaki tu katika nafasi ya kusambaza taarifa, bali zilifanya kazi kama vituo vya kutoa maagizo na kuelekeza hatua za uwanjani. Maelekezo kuhusu namna ya kutengeneza vilipuzi vya kienyeji kama molotov, mbinu za kushambulia taasisi za serikali, njia za kukusanyika, maeneo yasiyoonekana na kamera za ulinzi, na hata ratiba ya operesheni, yote yalipitishwa kupitia mitandao hiyo.

Katika mazingira kama hayo, intaneti iligeuka kuwa kiungo muhimu kati ya wahusika wa ndani ya nchi na vyumba vya uratibu vilivyokuwa nje ya mipaka, na hivyo kuwa chombo kikuu cha kuunganisha taarifa, maelekezo na mikakati.

Kutoka katika mtazamo wa kiusalama, hali hiyo ilikuwa karibu sana na muundo wa “mtandao wa ugaidi wa kimtandao” ,  mfumo ambao ndani yake watu binafsi au makundi madogo yaliyotawanyika nchini huendeshwa na kuungwa mkono kwa njia ya habari, fedha na taarifa za kijasusi kutoka nje, na hivyo kutekeleza vitendo vinavyovuka mipaka ya maandamano ya kiraia.

Basi lililoteketezwa na magaidi waliopata himaya ya tawala za Israel na Marekani

Katika mazingira kama hayo, kukata intaneti kulikuwa hatua ya kuzuia kuenea kwa vurugu na pia kuzuia upelekaji wa taarifa za kiutendaji kwenda nje ya nchi, taarifa ambazo zingeliwezesha uratibu wa operesheni na kuongeza hatari ya machafuko kupanuka.

Nchini Iran, hatua ya kukata intaneti mnamo Januari 2026 ilitekelezwa kwa utaratibu wa hatua kwa hatua na kwa malengo mahsusi.

Kwanza, vizuizi vilielekezwa kwenye majukwaa yaliyokuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuratibu operesheni. Baadaye, kadiri kiwango cha vurugu kilivyozidi na watu pamoja na makundi yenye silaha kuingia uwanjani, udhibiti huo ulipanuliwa ili kuzuia uwezekano wa kutuma picha, mahali walipo (location) na taarifa za moja kwa moja kwenda kwenye vyumba vya uratibu vilivyokuwa nje ya nchi.

Hatua hii ilisababisha mtikisiko mkubwa katika mtandao wa mawasiliano wa makundi yaliyokuwa yamepangwa. Uratibu mwingi ambao hapo awali ulifanyika ndani ya sekunde chache ulisimama kabisa, na makundi madogo ya ndani yaliyokuwa yakitegemea maelekezo kutoka nje yakapoteza uwezo wao wa kufanya operesheni.

Moja ya sababu kuu za mafanikio ya hatua hii ilikuwa utegemezi mkubwa wa mitandao ya kupindua serikali kwenye mawasiliano ya mtandaoni.

Tofauti na makundi ya jadi ya chini kwa chini ambayo huwa na muundo wa ngazi za siri na njia fiche za mawasiliano, mitandao mipya imejengwa hasa katika mazingira ya kidijitali. Bila mawasiliano ya papo kwa papo na vyanzo vyao vya nje, makundi haya hayana uwezo wa kufanya maamuzi kwa kujitegemea.

Kukata intaneti kuliwanyang’anya faida hiyo muhimu. Matokeo yake, operesheni nyingi zilizokuwa zikitegemea uratibu wa sekunde chache zilisitishwa nusu njiani au hazikuweza kuanza kabisa, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa makundi hayo kuendeleza shughuli zao.

Kwa upande mwingine, kukata intaneti kulipunguza pia uwezekano wa kusambaa kwa kiwango kikubwa kwa habari za uongo, picha zilizotengenezwa na simulizi zilizopangwa kwa makusudi.

Katika siku za mwanzo za machafuko, taarifa nyingi zisizo sahihi zilienezwa kwa lengo la kuchochea vurugu na kueneza hofu miongoni mwa umma. Kupitia udhibiti wa intaneti, mtiririko huu wa upotoshaji ulidhibitiwa kwa kiasi kikubwa, na vyombo vya habari vya ndani viliweza kutoa taswira iliyo sahihi zaidi ya kile kilichokuwa kikitokea.

Kukata intaneti mnamo Januari 2026 kulikuwa pia sehemu ya mkakati mpana wa kiusalama uliolenga kuzuia machafuko yasigeuke kuwa mgogoro kamili wa usalama wa taifa.

Ingawa hatua hiyo ilisababisha changamoto fulani kwa wananchi, kutoka katika mtazamo wa usalama wa kitaifa ilichangia kukatiza mawasiliano ya mitandao ya kupindua serikali na wale waliokuwa wakiwasaidia kutoka nje ya nchi, na hatimaye kusababisha kusambaratika kwa mfumo wao wa uratibu na uongozi.

Hatimaye, inaweza kusemwa kwamba uzoefu wa Iran katika kukabiliana na shambulio la kigaidi la hivi karibuni, pamoja na mifano kutoka nchi nyingine, unaonyesha wazi kuwa pale ambapo makundi ya kigaidi hutumia majukwaa ya mtandaoni kwa uratibu, propaganda na kuchochea vurugu, udhibiti wa muda wa intaneti unaweza kuwa hatua ya lazima, yenye uwajibikaji na ya kinga.

Lengo kuu la hatua kama hii si kukandamiza uhuru wa kimsingi, bali kuvuruga njama za maadui, kulinda mali ya umma na kuhakikisha usalama wa maisha ya watu wasio na hatia.