Waislamu Canada wataka kukomeshwa chuki dhidi ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136024-waislamu_canada_wataka_kukomeshwa_chuki_dhidi_ya_uislamu
Viongozi wa Waislamu nchini Canada wametoa wito wa kukomeshwa kwa matamshi ya chuki na uenezaji wa hofu dhidi ya Uislamu na Waislamu, huku nchi hiyo ikijiandaa kuadhimisha miaka tisa tangu kutokea shambulio baya dhidi ya msikiti katika mkoa wa Quebec.
(last modified 2026-01-29T09:11:31+00:00 )
Jan 29, 2026 06:36 UTC
  • Waislamu Canada wataka kukomeshwa chuki dhidi ya Uislamu

Viongozi wa Waislamu nchini Canada wametoa wito wa kukomeshwa kwa matamshi ya chuki na uenezaji wa hofu dhidi ya Uislamu na Waislamu, huku nchi hiyo ikijiandaa kuadhimisha miaka tisa tangu kutokea shambulio baya dhidi ya msikiti katika mkoa wa Quebec.

Stephen Brown, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada (NCCM), amesema maadhimisho hayo ya leo Alkhamisi ni ukumbusho wa taathira za chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

"Ni jambo ambalo kwa bahati mbaya linaua watu," Brown ameambia kanali ya Al Jazeera na kuongeza kuwa, “[Maadhimisho hayo] yanatulazimisha kukumbuka kwamba kuna matokeo mabaya haswa ya chuki."

Ikumbukwe kuwa, Waislamu wa kiume waliuawa baada ya kufyatuliwa risasi katika Kituo cha Utamaduni cha Kiislamu jijini Quebec mnamo Januari 29, 2017; shambulio hilo likihesabiwa kuwa baya zaidi dhidi ya maabadi katika historia ya Canada.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada amesema, "Mara tu baada ya mauaji ya msikiti wa jiji la Quebec, kulikuwa na hamu katika jamii ya kujaribu kurekebisha makovu na kujenga madaraja." 

Ameongeza kuwa, "Kwa bahati mbaya, kile ambacho watu wengi wanakiona [sasa] - na hasa Waislamu wanaoishi Quebec, ni kurejea kwa kiasi kikubwa chuki dhidi ya Uislamu na kueneza hofu dhidi ya Waislamu kwa maslahi ya kisiasa."

Mwaka 2024, Baraza la NCCM liliripoti kuongezeka kwa 1300% kwa matukio ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika nchi hiyo ya Amerika Kaskazini baada ya kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.