Canada kuitambua rasmi nchi ya Palestina mwezi Septemba mwaka huu
-
Mark Carney
Markk Carney Waziri Mkuu wa Canada ametangaza kuwa nchi hiyo imepanga kuitambua rasmi nchi ya Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu.
Mark Carney amekuwa na kikao na waandishi wa habari huko Ottawa ambapo ameashiria mateso yasiyovumilika wanayopitia watu wa Gaza na kusema: Canada imekusudia kuitambua rasmi nchi ya Palestina katika Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Globe and Mail, Carney ameongeza kwa kusema: "Uamuzi huu umefanywa kufuatia Mamlaka ya Ndani ya Palestina kujitolea kutekeleza mageuzi ya kimsingi na ahadi ya Rais wa serikali ya Mahmoud Abbas ya kutoifanya Palestina kuwa ya kijeshi na kuandaa uchaguzi mkuu mwaka 2026."
Awali, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer pia alisema Jumanne wiki hii kwamba atalitambua taifa la Palestina mwezi Septemba ikiwa utawala wa Israel hautakubali kusitishwa vita huko Gaza na kutumwa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.
Hivi karibuni pia Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema kuwa Paris itaitambua rasmi nchi ya Palestina na kwamba itatangaza rasmi uamuzi huu katika Mkutano wa Baraza Kuu la UN mwezi Septemba.