Trump aitishia Canada kwa ushuru wa 100%, kisa biashara na China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135868-trump_aitishia_canada_kwa_ushuru_wa_100_kisa_biashara_na_china
Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kuitoza Canada ushuru wa asilimia 100 iwapo Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney atatekeleza makubaliano ya kibiashara na China.
(last modified 2026-01-25T06:57:42+00:00 )
Jan 25, 2026 06:57 UTC
  • Trump aitishia Canada kwa ushuru wa 100%, kisa biashara na China

Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kuitoza Canada ushuru wa asilimia 100 iwapo Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney atatekeleza makubaliano ya kibiashara na China.

Katika taarifa aliyotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social jana Jumamosi, Trump alisema Carney "amekosea sana" ikiwa anafikiri Canada inaweza kuwa "bandari ya kupokea" kwa ajili ya China kutuma bidhaa zake nchini Marekani.

"Ikiwa Canada itatekeleza makubaliano hayo na China, itakumbwa mara moja na ushuru wa 100% kwa huduma na bidhaa zote za Canada zinazoingia Marekani," Trump ameandika katika ujumbe huo, ambapo alimtaja Carney kama "Gavana" badala ya Waziri Mkuu.

Vitisho vya Trump vinajiri katika hali ambayo, mvutano unazidi kuongezeka kati ya Canada na serikali ya Marekani, hususan kuhusu sera za biashara.

Carney amewahi kutoa ujumbe mzito kwa Marekani, akisema kwamba Ottawa haipaswi "kusahau usaliti wa Washington ambao umeathiri vibaya uhusiano wa kibiashara wa nchi hizo mbili."

Hivi karibuni, Msemaji wa Ikulu ya White House alitangaza kuwa Rais wa Marekani angali ana nia ya kuiunganisha Canada na ardhi ya nchi hiyo na kuigeuza kuwa jimbo la 51 la Marekani.