Maporomoko ya udongo yaongezeka Indonesia; waokoaji wapambana kunusuru watu waliokwama
-
Waokoaji wakitafuta manusura wa maporomoko ya udongo, Indonesia
Wafanyakazi wa huduma za uokoaji nchni Indonesia leo wameendelea kufanya juhudi kubwa ndani ya matope kufuatia maporoko ya udongo yaliyoikumba nchi hiyo kwa lengo la kutafuta makumi ya watu ambao hadi sasa bado hawajulikani walipo.
Maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku moja iliyopita kwenye kisiwa kikuu cha Java nchini Indonesia hadi sasa yamesababisha vifo vya takriban watu 11.
Maporomoko hayo ya udongo yaliyotokea jana alfajiri yaliathiri eneo la miteremko katika Mlima Burangrang katika mkoa wa Java Magharibi na kuzamisha ardhini nyumba 34 katika kijiji cha Pasir Langu.
Watu 79 hadi sasa hawajulikani walipo huku wengi wakihofiwa kuwa wamefunikwa na tani kadhaa za matope, miamba na miti iliyong'olewa na mafuriko.
Takriban watu 230 wanaoishi karibu na kijiji cha Pasir Langu wamehamishiwa kwenye makazi ya muda. Wafanyakazi wa uokoaji leo asubuhi walipata miili mingine miwili na hivyo kufanya idadi ya waliofariki dunia hadi sasa kufikia 11.
Picha za video zilizorushwa jana na Idara ya Huduma za Uokoaji ya Indonesia (Basarnas) zilionyesha wafanyakazi wa idara hiyo wakitumia suhula za shambani na mikono yao mitupu kuvuta mwili uliokuwa umefunikwa na tope kutoka ardhini.
Makamu wa Rais wa Indonesia, Gibran Rakabuming Raka, mapema leo ametembelea maeneo yaliyoathiriwa na maporomo ya udongo huko Java Mashariki na Bandung Magharibi na kuwaagiza maafisa husika kuchukua hatua kuzuia kujikariri matukio kama hayo.