Maandamano yashtadi US baada ya raia mwingine kuuawa Minneapolis
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135872-maandamano_yashtadi_us_baada_ya_raia_mwingine_kuuawa_minneapolis
Maajenti wa serikali kuu ya Marekani wamemuua kwa kumpiga risasi mtu mwingine mjini Minneapolis huku kukiwa na msako mkali dhidi ya wahamiaji, na kushadidisha maandamano na wito mpya kwa Rais Donald Trump kuwaondoa mara moja maafisa hao waliojizatiti kwa silaha katika jiji hilo lililoko katika jimbo la Minnesota.
(last modified 2026-01-25T06:59:04+00:00 )
Jan 25, 2026 06:59 UTC
  • Maandamano yashtadi US baada ya raia mwingine kuuawa Minneapolis

Maajenti wa serikali kuu ya Marekani wamemuua kwa kumpiga risasi mtu mwingine mjini Minneapolis huku kukiwa na msako mkali dhidi ya wahamiaji, na kushadidisha maandamano na wito mpya kwa Rais Donald Trump kuwaondoa mara moja maafisa hao waliojizatiti kwa silaha katika jiji hilo lililoko katika jimbo la Minnesota.

Kamanda Mkuu wa Polisi mjini Minneapolis, Brian O’Hara amewaambia waandishi wa habari kwamba, mwanamume huyo aliyekuwa na umri wa miaka 37 alifariki dunia hospitalini jana Jumamosi, baada ya kupigwa risasi mara kadhaa.

Mkazi huyo wa Minneapolis alikuwa raia wa Marekani, O’Hara ameeleza bayana. Wazazi wa mwanamume huyo walimtambua kama Alex Pretti, muuguzi wa kitengo cha wagonjwa mahututi.

Mauaji hayo yanajiri baada ya kupelekwa kwa maajenti wa uhamiaji na askari wengine wa serikali ya shirikisho ya US huko Minneapolis, ambapo wamekuwa wakifanya msako kama sehemu ya juhudi za Trump za kukabiliana na uhamiaji.

Aidha yametokea huku maandamano yakifanyika karibu kila siku huko Minneapolis na miji mingine, tangu kujiri mauaji ya Renee Good, mwanamke wa Kimarekani na mama wa watoto watatu aliyekuwa na umri wa miaka 37, ambaye aliuawa pia wakati afisa wa Uhamiaji na Forodha (ICE) alimpofyatulia risasi akiwa kwenye gari lake.

Meya wa Minneapolis, Jacob Frey amelaani mauaji hayo na kukosoa vikali uwepo wa maafisa usalama wa serikali ya shirikisho katika jiji hilo, akitaka kusitishwa kwa operesheni hiyo, na kumtaka Trump kuwaondoa maafisa hao huko Minneapolis mara moja.

Meya huyo akimhutubu Trump kwa masitiko amehoji, "Ni wakazi wangapi zaidi, ni Wamarekani wangapi zaidi, wanaopasa kufa au kuumia vibaya ili operesheni hii ikome?"