Brigedia Jenerali Vahidi: Tumejiandaa kutoa jibu kali kwa chokochoko za maadui
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, amesema Iran itatoa jibu kali kwa uchokozi na uvamizi wowote wa maadui zake.
Akizungumza katika sherehe ya kitaifa ya kuwaenzi mashahidi kutoka Mkoa wa Azerbaijan Magharibi, iliyofanyika katika makao makuu ya jimbo hilo, Orumiyeh jana Jumamosi, afisa huyo wa kijeshi alisema njama za maadui kuishinda Iran ziligonga mwamba wakati wa vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na Israel mwezi Juni 2025 na machafuko ya hivi karibuni hapa nchini.
"Tuko tayari kutoa jibu kali kwa hatua yoyote ya kichokozi ya maadui sugu wa taifa la Iran," Brigedia Jenerali Vahidi amesisitiza.
Amebainisha kuwa, maadui walishindwa vikali wakati wa vita vya siku 12 na walijaribu kufidia kwa kusababisha uchochezi wakati wa machafuko ya hivi karibuni. Kwa mara nyingine tena, walishindwa vikali kutokana na umoja na mshikamano wa watu wa Iran, aliongeza. Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la Iran aidha amesema Marekani na washirika wake wanafanya juu chini kuigawanya Iran ili waweze kuidhibiti.
Kabla ya hapo, Jenerali Mohammad Pakpour, Kamanda Mkuu wa jeshi la SEPAH alizionya Marekani na Israel dhidi ya kufanya "mahesabu yoyote ghalati mkabala wa Iran"
Jenerali Pakpor amesema, "Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Iran wapo tayari zaidi kuliko hapo awali, kidole kipo kwenye kitufe, tayari kutekeleza maagizo na amri ya Amiri Jeshi Mkuu."
Makamanda wa Iran wanasisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itajibu kwa nguvu zote uchokozi wa maadui, na kwamba kambi zote za Marekani katika eneo la Asia Magharibi zitakuwa shabaha halali ya Iran iwapo italishambulia taifa hili.