Shambulio la droni la Israel laua watoto 2 Gaza
Watoto wawili wameuawa shahidi katika shambulio la Israel kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, katika ukiukaji wa hivi karibuni wa makubaliano ya kusitisha mapigano baina ya utawala huo katili na Harakati ya Muqawama ya Hamas katika eneo hilo la Wapalestina linalokaliwa kwa mabavu.
Vyanzo vya hospitali huko Gaza jana Jumamosi vilisema kuwa, watoto hao wa familia moja waliuawa wakati ndege isiyo na rubani ya Israel ilipowashambulia raia waliokuwa wakikusanya kuni karibu na Hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza.
Uhaba mkubwa wa fueli umewalazimisha Wapalestina wengi kutafuta nishati mbadala popote wanapoweza, huku wakikabiliwa na wimbi la baridi kali.
Wapalestina wanaoishi katika mahema ya muda hawana ulinzi kutokana na upepo mkali unaovuma na mvua, kwani makazi mengi yametengenezwa kwa turubai nyembamba na karatasi za plastiki.
Israel inaendelea kuzuia misaada muhimu inayoingia katika eneo hilo, kama vile mahema, suhula au vifaa vya kurekebisha mahema, kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo ilifikia na Hamas mnamo Oktoba 2025, pamoja na majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa kama utawala ghasibu katika Ukanda huo.
Wakati huo huo, Amjad Al-Shawa, Mkuu wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, ameiambia Kanali ya Televisheni ya Al Jazeera kwamba hali ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo imekuwa ngumu na ngumu zaidi.
Mkuu wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina ameongeza kuwa kwa uchache watu 18,500 wanahitaji matibabu ya haraka nje ya Gaza.