Usitishaji vita wa kimaonyesho Gaza; kifuniko cha Wazayuni cha kuendeleza jinai
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135888-usitishaji_vita_wa_kimaonyesho_gaza_kifuniko_cha_wazayuni_cha_kuendeleza_jinai
Mkurugenzi wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina ameonya kuhusu kuendelea kuuawa raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-01-25T16:07:39+00:00 )
Jan 25, 2026 11:55 UTC
  • Usitishaji vita wa kimaonyesha Gaza; kifuniko cha Wazayuni cha kuendeleza jinai
    Usitishaji vita wa kimaonyesha Gaza; kifuniko cha Wazayuni cha kuendeleza jinai

Mkurugenzi wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina ameonya kuhusu kuendelea kuuawa raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Ajith Sunghay, mkurugenzi wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina ameonya dhidi ya kuendelea kuuawa raia wa Palestina na kusema: "Jamii ya kimataifa lazima iongeze usaidizi na mashinikizo ili kukomesha umwagaji damu, kuboresha hali ya haki za binadamu, na kujenga upya Gaza." Kabla yah apo, Amjad Al-Shawa, mkuu wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, aliiambia Kanali ya Televisheni ya Al Jazeera kwamba hali ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo imekuwa ngumu na ngumu zaidi.

Mkuu wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina aliongeza kuwa angalau watu 18,500 wanahitaji matibabu ya haraka nje ya Gaza.

Salah Abdel Ati, Mkuu wa Kamisheni ya Kimataifa ya Ulinzi wa Haki za Wapalestina (Hashd), pia alizungumzia mauaji ya waandishi wa habari watatu yaliyofanywa na wavamizi wa Kizayuni na kusema: "Kuuawa shahidi waandishi hao wa habari watatu kunaonyesha kwamba, makubaliano ya kusitisha mapigano si tu kwamba, hayajatoa ulinzi wowote kwa raia, bali yamekuwa kifuniko cha mauaji yanayoendelea na kulenga raia moja kwa moja."

Abdul-Ati aliongeza: "Kuendelea kulengwa raia na waandishi wa habari huko Gaza, pamoja na kulazimishwa kuhama makazi yao na sambamba na uharibifu wa miundombinu, ni uthibitisho dhahiri wa mauaji ya kimbari, yanayofanywa kwa njia nyingi na chini ya kimya cha kimataifa."

Mashirika mengi ya haki za binadamu, wataalamu wa Umoja wa Mataifa, na mashirika yasiyo ya kiserikali yameonya mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni kwamba, makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza kivitendo yameshindwa kuzuia kuendelea mashambulizi na ukiukwaji wa haki za raia.

Licha ya kupita majuma mengi tangu kutangazwa usitishaji mapigano huko Gaza, lakini ushahidi wa nyanjani na ripoti kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu zinaonyesha kwamba, usitishaji mapigano huo sio tu kwamba, haujapelekea kupungua vitendo vya utumiaji mabavu, bali katika visa vingi umekuwa wenzo wa wa Wazayuni wa kuendeleza mashambulizi na hivyo kushadidisha mashinikizo dhidi ya raia. Vifo vya waandishi wa habari hao watatu ni moja tu ya mifano ya hivi karibuni ya ukiukaji wa usitishaji mapigano ambao kwa mara nyingine tena umeonyesha kutokuwa na utendaji mbinu na mikakakati ya kimataifa katika kuwalinda raia huko Gaza.

Uungaji mkono wa kisiasa na kijeshi wa madola ya Magharibi hususan Marekani kwa utawala wa Kizayuni, kutumia haki ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuzuia kupasishwa maazimio ya kisheria na mashinikizo ya kutosha ya kuzuia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kumeruhusu kuendelea bila kizuizi vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Uungaji mkono huu umechafua anga inayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa usitishaji mapigano wa dhati na wa kweli.

Mamia ya shule zimebomolewa katika Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulio ya jeshi la utawala haramu wa Israel 

 

Ukweli wa nyanjani huko Gaza unaonyesha kwamba, usitishaji mapigano umekuwa wa machaguo na wenye mipaka maalumu. Mashambulizi ya anga na ardhini yanaendelea katika baadhi ya maeneo, waandishi wa habari wamelengwa, na miundombinu muhimu inaendelea kuharibiwa.

Mojawapo ya vipengele vikubwa vya mgogoro huu ni ukimya na kushindwa taasisi za kimataifa kutetea haki halali za Wapalestina. Ingawa serikali za Magharibi zinatoa matamko ya kisiasa kuunga mkono usitishaji mapigano, lakini hakuna hatua kali na za vitendo zinazochukuliwa na mataifa. Ombwe hili, na kutochukua hatua Marekani na serikali za Magharibi, kulingana na wanaharakati wengi wa haki za binadamu, limefungua njia ya kuendelea unyama wa utawala wa Kizayuni huko Gaza.

Matukio ya hivi karibuni huko Gaza yanaonyesha kwamba, usitishaji mapigano kivitendo umekuwa kifuniko cha mashambulizi yanayoendelea na ukiukwaji mkubwa wa haki za raia. Kuuawa shahidi waandishi wa habari, mauaji yanayoendelea ya watu wasio na ulinzi, uharibifu wa miundombinu muhimu, na mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka yote hayo yanaonyesha kwamba, utawala wa Kizayuni unaendelea na vitendo vyake vya kinyama bila kizuizi chochote.

Weledi wa mambo wanaamini kwamba, madhali hakuna nia na azma thabiti ya kimataifa ya kutoa shinikizo linalofaa ili kusimamisha kabisa mashambulizi ya utawala wa Israel, na kuhakikisha utekelezaji mzuri wa usitishaji mapigano, mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu huko Gaza utaendelea kushuhudiwa. Hali hii haionyeshi tu kutokuwa na maana yoyote mifumo ya kimataifa, lakini pia inafanya kuwa jambo la dharura kufikiria upya utendaji wa kimataifa kuhusiana na mgogoro wa Palestina.