Mwendesha Mashtaka wa Sudan: Tumewafungulia kesi mamluki 122 wa kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135886-mwendesha_mashtaka_wa_sudan_tumewafungulia_kesi_mamluki_122_wa_kigeni
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Sudan ameeleza kuwa kesi za jinai zimefunguliwa dhidi ya takriban mamluki 122 wa kigeni wanaopigana bega kwa bega na wanamgambo waasi wa Rapid Support Forces (RSF), huku watoto 135 waliosajiliwa kama wapiganaji katika vita hivyo wakirejeshwa kwa familia zao.
(last modified 2026-01-25T11:44:14+00:00 )
Jan 25, 2026 11:44 UTC
  • Intisar Ahmed Abdel Mutaal
    Intisar Ahmed Abdel Mutaal

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Sudan ameeleza kuwa kesi za jinai zimefunguliwa dhidi ya takriban mamluki 122 wa kigeni wanaopigana bega kwa bega na wanamgambo waasi wa Rapid Support Forces (RSF), huku watoto 135 waliosajiliwa kama wapiganaji katika vita hivyo wakirejeshwa kwa familia zao.

Bi Intisar Ahmed Abdel Mutaal ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi wa Jinai amesema kuwa baadhi ya mamluki tayari wamehukumiwa kifo. Mamlaka za Sudan zinaituhumu RSF kuwa imeajiri wapiganaji wa kigeni kutoka Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Colombia.

Ameongeza kuwa kamati yake imerekodi kesi za jinai 188,405 tangu kuanza vita vya ndani nchini sudan, huku baadhi ya kesi hizo zikihamishiwa katika mahakama maalumu. 

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Sudan amesema, Kamati ya Uchunguzi wa Jinai imepata ushahidi wa kuhusu ushirikiano wa Umoja wa Falme za Kiarabu na misaada yake kwa wanamgambo waasi. Amesema pia imethibitika kwamba nchi nyingine ziliruhusu silaha kuvushwa kupitia katika mipaka yao na kwenda kwa waasi hao. Itakumbuka kuwa UAE awali ilikanusha kuwaunga mkono wanamgambo wa RSF.

Abdel Mutaal amekituhumu kikosi cha RSF kuwa kimehusika na udhalilishaji wa kingono wa kifumo ikiwa ni pamoja na kuwadhalilisha kingono watoto na kwamba watoto 135 wamerejeshwa kwa familia zao kupitia Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu. 

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Sudan ametoa maelezo ya kina kuhusu  vitendo vya uhalifu vinavyodaiwa kufanywa dhidi ya kabila la Masalit huko El Geneina na mashambulizi ya RSF huko Kadugli na Dilling ambayo yaliua watu 114, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa kwa makombora shule ya chekechea wakati wa sherehe ya kuhitimu masomo.

Januari 19 mwaka huu Mahakama ya Kupambana na Ugaidi ya PortSudan ilianza kusikiliza kesi za washtakiwa 201, akiwemo kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo na Waziri Mkuu wa zamani Abdalla Hamdok, kwa tuhuma za kuchochea vita na kuhujumu mfumo wa katiba.