Pande za kisiasa Sudan kuunda muungano mpya ili kurejesha utawala wa kiraia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135846-pande_za_kisiasa_sudan_kuunda_muungano_mpya_ili_kurejesha_utawala_wa_kiraia
Makundi ya kisiasa ya Sudan ambayo yamejitenga na muungano mkuu wa demokrasia yamesema kuwa yanafanya juhudi za kuunda muungano mpana unaolenga kurejesha utawala wa kiraia nchini humo baada ya karibu miaka minne ya serikali inayoongozwa na jeshi.
(last modified 2026-01-24T13:04:50+00:00 )
Jan 24, 2026 13:04 UTC
  • Wanasiasa Sudan kuunda muugano wa utawala wa kiraia
    Wanasiasa Sudan kuunda muugano wa utawala wa kiraia

Makundi ya kisiasa ya Sudan ambayo yamejitenga na muungano mkuu wa demokrasia yamesema kuwa yanafanya juhudi za kuunda muungano mpana unaolenga kurejesha utawala wa kiraia nchini humo baada ya karibu miaka minne ya serikali inayoongozwa na jeshi.

Muungano huo unakutanisha pamoja harakati zilizokuwa zimejitenga na wapiganaji kwa jina la  Forces for Freedom and Change (FFC) baada ya jeshi la Sudan kushika hatamu za uongozi Oktoba 2021 na kuzuka vita kati ya jeshi na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), Aprili 2023.

Kundi moja ndani ya Chama cha Taifa cha Umma (NUP) kinachoongozwa na Mohamed Abdalla al-Doma na kundi la National Current linalojumuisha wanachama wa zamani wa Chama cha Congress ya Sudan vimefanya mkutano ili kuendeleza ajenda hiyo.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, chama cha NUP kimeganyika katika makundi matatu; kundi moja linaongozwa na mwenyekiti, Burma Nasir, ambalo linawaunga mkono wanamgambo wa RSF, huku kundi jingine linaloongozwa na al Doma likiliunga mkono jeshi la Sudan. Kundi la tatu linaongozwa na Katibu Mkuu al- Watheiq al-Berir ambalo linapinga vita.  

Mkutano huo wa makundi ya kisiasa Sudan umejadili suala la kumaliza vita, kuanzisha serikali ya mpito na kujenga maelewano ya kitaifa kuelekea utawala wa kiraia. Washiriki pia wamejadili mipango ya amani ya kijamii na kukomesha matamshi ya chuki.

Maafisa kutoka pande zote mbili wamesema kuwa wamefikia makubaliano ya kuratibu juhudi na kuendeleza mawasiliano na makundi mengine ya kisiasa ili kujenga harakati ya kiraia iliyojikita katika mazungumzo shirikishi ya amani  yanayoongozwa na Wasudani wenyewe.