Albanese: Israel ifukuzwe UN kwa kubomoa makao makuu ya UNRWA
Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ameilaani Israel kwa kubomoa makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) katika mji wa Baitul Muqaddas Mashariki unaokaliwa kwa mabavu, na kutaka kusimamishiwa unachama utawala huo wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye tovuti ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR), Francesca Albanese ameelezea ubomoaji huo kama "shambulio la kimfumo" kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa na taifa la Palestina.
"Nimeshtushwa na uharibifu unaoendelea kufanywa na Israel bila kizuizi chochote, kwani Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa zinabomolewa matofali kwa matofali mbele ya macho ya ulimwengu. Kushambulia UNRWA kunawakilisha kukanyagwa kwa juhudi za jamii ya kimataifa za kulinda maisha ya Wapalestina," amesema mwanadiplomasia huyo wa UN.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani kitendo hicho cha vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel cha kubomoa majengo yaliyomo ndani ya eneo la makao makuu ya Shirika la UNRWA.
Mwezi uliopita, Bunge la Israel, Knesset lilipitisha sheria ya kukata umeme na usambazaji wa maji kwa majengo ya UNRWA yaliyoko Baitul Muqaddas Mashariki.
Huko nyuma pia, Israel ilichukua hatua kama hizo za uadui dhidi ya UNRWA. Mnamo mwaka 2024, Knesset ilipitisha sheria ya kupiga marufuku shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa huko Israel, ikidai kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walihusika katika matukio ya Oktoba 7, 2023, madai ambayo shirika hilo limeyakanusha.
Umoja wa Mataifa umesema shirika la UNRWA linafungamana na msingi wa kutoegemea upande wowote, na kwa msingi huo linapasa kuheshimiwa.