Ripoti: Netanyahu hakuenda Davos kutokana na hofu ya kukamatwa
-
Netanyahu na Gallant
Vyombo vya habari vya utawala wa Israel vimeripoti kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hakuhudhuria Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos wiki hii kutokana na wasiwasi kwamba angeweza kukamatwa nchini Uswisi kufuatia hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Vyombo hivyo vya habari vimeripoti habari hiyo na kubainisha kwamba rais wa utawala huo, Isaac Herzog, alimwakilisha Netanyahu katika mkutano huo.
Katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, Herzog alilalamikia kutokuwepo kwa maafisa wa Israel katika jukwaa hilo na akatoa wito wa kuondolewa kwa hati za kukamatwa zilizotolewa na ICC dhidi ya maafisa wa Israel.
Hata hivyo, Herzog hakugusia sababu zilizopelekea kutolewa kwa hati hizo za kukamatwa zinazomlenga Netanyahu na Yoav Gallant, aliyekuwa waziri wake wa vita. Wawili hao wanasakwa na ICC kutokana na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu waliotenda katika Ukanda wa Gaza.
Uhalifu huo unatokana na vita ambavyo utawala wa Israel umeendesha dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023, vita ambavyo vimetajwa na wachambuzi wengi kama vya kinyama na vya mauaji ya kimbari, na ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 71,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliyotoa hati hizo mwaka 2024, kulikuwa na misingi ya kutosha kuamini kwamba wawili hao walihusika na uhalifu mbalimbali, ikiwemo kutumia njaa kama mbinu ya kivita, kuelekeza mashambulizi kwa makusudi dhidi ya raia, pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu kama vile mauaji, mateso ya kimfumo na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu.
Hati za kukamatwa zilizotolewa na ICC zimesambazwa kwa nchi 125 wanachama wa Mkataba wa Roma, ambao ndio ulioweka msingi wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Nchi hizo zina wajibu wa kisheria kumkamata Netanyahu na Gallant iwapo wataingia katika maeneo yao. Uswisi, mwenyeji wa mkutano wa Davos, ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba huo.
Tangu kuanza kwa vita, uwepo wa maafisa mbalimbali wa Israel, wanajeshi na hata timu za michezo katika mataifa tofauti umekuwa ukichochea maandamano makubwa ya wananchi wanaopinga ukatili wa utawala huo na kutaka waliowajibika wakamatwe na kufikishwa mahakamani.