UN yatoa wito mpya wa kutokomeza ukoloni
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136728-un_yatoa_wito_mpya_wa_kutokomeza_ukoloni
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ingawa zaidi ya mataifa 100 yamepata uhuru tangu mwaka 1945, mchakato wa kuondoa ukoloni bado haujakamilika. Ametoa kauli hiyo akifungua kikao cha mwaka 2026 cha Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Kutokomeza Ukoloni,
(last modified 2026-02-17T10:39:58+00:00 )
Feb 17, 2026 10:39 UTC
  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ingawa zaidi ya mataifa 100 yamepata uhuru tangu mwaka 1945, mchakato wa kuondoa ukoloni bado haujakamilika. Ametoa kauli hiyo akifungua kikao cha mwaka 2026 cha Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Kutokomeza Ukoloni,

Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 1960 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa linapitisha maazimio ya kutokomeza hali ya nchi kutojitawala ambapo hadi sasa maeneo hayo kwa sasa yanasimamiwa na Uingereza, Marekani na Ufaransa.

Katika hotuba yake iliyosomwa Jumatati kwa niaba na Courtenay Rattray ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu, Guterres ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Bermuda, Guam, Polinesia ya Ufaransa na Sahara Magharibi barani Afrika.

Katibu Mkuu ametaja vipaumbele vitatu vya kunasua maeneo hayo 17 kutoka mtego wa kutawaliwa, nayo ni: mazungumzo jumuishi kati ya maeneo husika na mataifa yanayoyasimamia; ushiriki mkubwa zaidi wa vijana katika kuamua mustakabali wao wa kisiasa; na hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa maeneo ya visiwa vidogo yanayokabiliwa na kupanda kwa kina cha bahari na hali mbaya ya hewa.

Aidha, amegusia madhara ya muda mrefu ya ukoloni, yakiwemo unyonyaji wa kiuchumi na ukosefu wa usawa wa kimfumo, akizihimiza nchi wanachama kuharakisha juhudi za kufanikisha haki ya kweli ya kujitawala.

Mjumbe kutoka Venezuela, akiwakilisha nchi 24 za Kundi la Marafiki wa kulinda Chata ya Umoja wa Mataifa amesema, “mwezi Novemba mwaka jana tuliandikia barua kamati hii tukitaka kupata maendeleo ya utekelezaji wa jukumu lake kuu la kutokomeza ukoloni.”

Naye mjumbe kutoka Ofisi ya uwakilishi wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa amegusia azimio namba 1514 la Baraza Kuu la kutaka nchi zinazomilikiwa zipatiwe uhuru na kusema  “ujumbe wangu unasalia umejizatiti kuunga mkono juhudu za Umoja wa Mataifa za kutokomeza ukoloni kwa kuwa utokomezaji wa ukoloni  bado ni kipaumbele kikuu cha kazi za shirika.”

Amekumbusha kuwa nchi zinazotawaliwa bado zinaendelea kukabiliwa na changamoto lukuki kama zile za mazingira, uchumi, kijamii, kitamaduni na kisiasa.