Kwa nini rais wa Brazil amemkejeli Trump?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135820-kwa_nini_rais_wa_brazil_amemkejeli_trump
Rais Lula da Silva wa Brazil amemkejeli Rais Donald Trump wa Marekani kutokana na tweet nyingi za kutatanisha anazoandika katika mitandao ya kijamii.
(last modified 2026-01-24T02:47:30+00:00 )
Jan 24, 2026 02:47 UTC
  • Kwa nini rais wa Brazil amemkejeli Trump?

Rais Lula da Silva wa Brazil amemkejeli Rais Donald Trump wa Marekani kutokana na tweet nyingi za kutatanisha anazoandika katika mitandao ya kijamii.

Da Silva amemkejeli Trump kwa kumwambia kuwa anataka kutawala dunia kupitia Twitter ambayo kwa sasa inaitwa X. Awali Da Silva alilaani hatua ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na kuiona kuwa ni dharau na kukosea heshima mamlaka ya nchi hiyo na kuvuka "mistari isiyokubalika". Huku akilaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na kutekwa nyara Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo, Da Silva amesisitiza kwamba hatua hii ilivuka "mstari mwekundu usiokubalika". Rais wa Brazil ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Vitendo hivi ni tusi kubwa kwa uhuru wa Venezuela na mfano hatari sana kwa jamii nzima ya kimataifa." Shirika la habari la Reuters limeongeza kuwa Da Silva ametaka hatua "kali" ichukuliwe na Umoja wa Mataifa dhidi ya Marekani kutokana na uvamizi wake huo.

Akigusia tabia ya Donald Trump katika vyombo vya habari, Da Silva, ambaye ana uzoefu na historia ndefu katika siasa, amesisitiza mara kwa mara kwamba mwanasiasa mzuri anapaswa kuzungumza kwa umakini na kuwajibika mbele ya maoni ya umma, badala ya kuchapisha jumbe kila baada ya dakika chache ambazo zinajibu masuala ya wakati huo kuliko kuakisi misimamo rasmi ya rais wa nchi. Tofauti hii ya mbinu imemfanya wakati mwingine kukejeli tabia ya Trump ya Twitter.

Katika muhula wake wa kwanza wa urais Trump alitumia Twitter na sasa mtandao wa kijamii wa Truth Social, ambao aliuanzisha mwenyewe Februari 2022, kama njia yake kuu ya mawasiliano. Kuanzia masuala ya usalama wa taifa hadi kashafa za mtu binafsi, anachapisha na kutangaza kwa kasi na sauti kubwa anachokitaka katika mitandao hiyo. Kwa mfano, katika siku moja anaweza kuchapisha tweet kadhaa kuhusu uchumi wa Marekani, zikiwemo zile zinazohusiana na ukuaji wa soko la hisa na uendeshaji wake, au kutishia makampuni makubwa kwamba iwapo yatahamishia viwanda vyao nje ya nchi, yatakabiliwa na ushuru mkubwa. Siku hiyo hiyo, anaweza kuandika tweet nyingine zinazohusiana na uhamiaji na kutetea ukuta wa mpakani, kisha ghafla akaingia kwenye hoja tofauti kabisa, akiandika kuhusu vyombo vya habari na kuvituhumu kuwa vinaeneza "habari bandia."

Trump

Wingi huu wa jumbe, ambao wakati mwingine hufikia makumi ya tweet kwa siku, umewashangaza viongozi wengi wa dunia. Da Silva amekuwa akisema mara kwa mara kwamba mwanasiasa anapaswa kuwa na muda wa kufikiria na kutangaza maamuzi yake katika mfumo wa sera rasmi, na sio kuchapisha kila hisia ya wakati maalum kupitia jumbe za mtandaoni. Amehoji katika moja ya hotuba zake kwamba "ikiwa rais wa nchi kubwa atatweet sana kila siku, basi ataiongoza lini nchi?" Tabia hii ya Trump ndiyo imemfanya awe mada inayofaa ya kukosolewa na kukejeliwa.

Trump pia hutweet kuhusu masuala ya kimataifa kwa kasi na mhemko huo huo. Huchapisha mfululizo wa jumbe kuhusu viongozi wa nchi nyingine katika dmuda mfupi sana. Wakati mmoja huzungumzia uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na nchi fulani na dakika chache baadaye kuitishia nchi hiyo hiyo. Kwa wanasiasa kama Da Silva, wanaoamini diplomasia na mazungumzo ya nyuma ya pazia, tabia hii ni ishara ya kiongozi kutokuwa na utulivu na kutotabirika.

Kando na hayo, Trump ameendelea kutumia Twitter kuwashambulia wapinzani wake wa ndani. Amewahutubu wawakilishi wa Congress, magavana, wanahabari na hata waliokuwa wanachama wa serikali yake kwa maneno makali. Mtindo huu wa mawasiliano, ambao unaonekana zaidi kuwa mjadala wa mtandaoni kuliko tabia ya rais, unachukuliwa na Da Silva na viongozi wengine wengi wa dunia kuwa usio wa kawaida na hata wa kuchekesha.

Kwa ujumla, kinachomfanya Da Silva amkejeli Trump sio tu idadi kubwa ya tweet anazotuma, bali namna anavyotumia chombo hicho cha mawasiliano, kwa kadiri kwamba ameondoa kabisa mipaka inayotenganisha sera rasmi za serikali na matakwa yake binafsi. Kwa rais wa Brazil, tabia hii ni kielelezo cha siasa na hisia za pupa, jambo ambalo ni ishara ya siasa za kushangaza za uongozi wa Trump katika zama hizi.