Kamanda: Iran itatoa majibu makali kwa vitisho vya Trump
-
Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi, kamanda wa Kitengo cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)
Kamanda mwandamizi wa jeshi la Iran amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu iko tayari na ina hakika itajibu kwa nguvu vitisho na kauli za Rais wa Marekani, Donald Trump.
Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi, kamanda wa Kitengo cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), alitoa kauli hizo pembezoni mwa mkutano uliowakutanisha viongozi wa zamani na wa sasa wa jeshi hilo. Mkutano ulifanyika Ijumaa katika kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Alisema kwamba, “Trump anazungumza sana, lakini anapaswa kuwa na hakika kwamba atapata jibu lake katika medani ya vita.”
Kauli hizo zilitolewa kufuatia ongezeko la vitisho kutoka kwa Trump, aliyedai kwamba Marekani itachukua hatua mpya za kijeshi dhidi ya Iran endapo Jamhuri ya Kiislamu itakabiliana na watu waliokuwa wakiibua ghasia na machafuko nchini baada ya kuteka maandamano ya kiuchumi.
Vikosi vya usalama vya Iran vilithibitisha kwamba vinara wa ghasia hizo walipokea mafunzo, silaha na msaada wa kimkakati kutoka Marekani na Israel. Maafisa wa Iran wameahidi kushughulikia changamoto za kiuchumi za taifa, lakini wakati huohuo wameapa kusimama imara dhidi ya juhudi zozote za kuyageuza maandamano yanayohusiana na masuala ya kiuchumi kuwa vurugu na machafuko.
Kamanda huyo amebainisha kuwa uzalishaji wa vifaa vya anga katika sekta mbalimbali umeongezeka kwa kiwango kikubwa tangu vita vya siku 12 wakati utawala haramu wa Israel, kwa msaada wa Marekani ulianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka jana. Jenerali Mousavi amesema kuwa udhaifu uliojitokeza wakati wa vita hivyo umechunguzwa kikamilifu na kurekebishwa ipasavyo, akisisitiza kwamba, “Kitengo cha Anga cha IRGC kwa sasa kipo katika kilele cha utayari wake wa kiulinzi.”