Ubepari; unyonyaji wa maliasili na shinikizo kwa mazingira
Ubepari, kama mojawapo ya mifumo mikuu ya kiuchumi katika ulimwengu wa sasa, umeundwa kwa kuzingatia ulimbikizaji wa mtaji, faida na upanuzi wa masoko usio na kikomo.
Ingawa mfumo huu umeimarisha teknolojia na kuongeza uzalishaji katika baadhi ya maeneo, lakini umekita mizizi katika unyonyaji wa maliasili na kutoa mashinikizo makubwa dhidi ya mazingira. Uhusiano wa ubepari na mazingira umejengeka katika msingi wa unyonyaji, ambapo mazingira hayachukuliwi kama mfumo wa ikolojia hai, bali kama chombo cha kukamuliwa na chanzo kisicho na mwisho cha faida nono. Mtazamo huu ndio chanzo cha migogoro mingi ya kimazingira leo duniani.
Moja ya vipimo muhimu vya suala hili ni kasi isiyo ya kawaida ya uchimbaji wa maliasili. Katika mfumo wa kibepari, ukuaji wa uchumi lazima uwe wa kudumu na wa kasi ya juu. Ukuaji huu hauwezi kutimia bila kuwepo matumizi zaidi ya nishati, maji, ardhi, misitu na madini. Ili kudumisha faida, makampuni makubwa huamua kuchimba migodi kiholela, ambapo mchakato huu husababisha uharibifu mkubwa wa misitu, mmomonyoko wa udongo, kupunguza viumbe hai na kuharibu makazi asilia ya wanyama na wadudu. Ukataji wa miti katika msitu wa Amazon, uchimbaji mafuta kupita kiasi katika maeneo nyeti, na vilevile kuchimba madini kiholela barani Afrika ni mifano ya wazi ya mwelekeo huu.
Mwelekeo mwingine ni uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa unaosababishwa na uzalishaji wa viwandani. Kwa kuhimiza uzalishaji na matumizi makubwa ya bidhaa, ubepari huzalisha kiasi kikubwa cha taka za viwandani, kemikali na plastiki. Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli zao, viwanda vingi hupuuza viwango vya mazingira safi na kuitwisha jamii hewa, maji na udongo uliochafuka kama "gharama za nje." Uchafuzi huu sio tu hutishia afya ya wanadamu, lakini pia huvuruga mzunguko asilia wa dunia. Ongezeko la joto duniani, gesi chafuzi na mabadiliko ya hali ya hewa ni matokeo ya moja kwa moja ya mantiki hii mbovu ya kuzingatia faida tu bila kujali afya na maslahi ya wanadamu pamoja na viumbe wengine duniani.
Ubepari pia unakuza matumizi ya bidhaa kama thamani ya kiutamaduni. Matangazo mengi huhimiza watu kununua zaidi bidhaa na kuvibadilisha haraka. Mzunguko huu usio na mwisho wa matumizi ya bidhaa huongeza hitajio la uzalishaji zaidi na matokeo yake ni mashinikizo zaidi kwenye maliasili na kuharibiwa mazingira. Bidhaa ambazo zina umri mfupi au zimeundwa kwa makusudi kuharibika haraka huongeza kiasi cha taka za elektroniki na viwandani, na hivyo kufanya udhibiti wa taka hizi kuwa tatizo la mazingira.
Suala jingine muhimu ni kutokuwepo usawa wa kimazingira. Katika mfumo wa kibepari, nchi tajiri na makampuni makubwa hunufaika zaidi na maliasili, huku nchi maskini na jamii zilizotengwa zikiachwa ziteseke. Kwa kawaida nchi na maeneo maskini ndiyo huwa sehemu za kuhamishia na kufukiwa taka hatarishi, uchimbaji madini haribifu au viwanda vinavyochafua mazingira. Ukosefu huu wa usawa hupelekea migogoro ya mazingira kuwa migogoro ya kijamii na kibinadamu.
Matokeo ya mwenendo huu ni makubwa na hatari mno. Matokeo ya kwanza ni kuongezeka kwa mabadiliko ya hali ya hewa. Ongezeko la halijoto, kuyeyuka barafu katika maeneo yenye baridi kali duniani, kupanda kwa kina cha bahari na kudhihiri kwa majanga ya hali ya hewa kama mafuriko, ukame na dhoruba ni matokeo ya moja kwa moja ya matumizi mabaya ya nishati ya mafuta, hasa katika nchi zilizoendelea pamoja na uharibifu wa misitu. Mabadiliko haya sio tu yanatishia mifumo ikolojia, bali pia yanahatarisha usalama wa chakula, rasilimali za maji na afya ya wanadamu.
Madhara mengine ni kupunguzwa kwa bioanuwai. Maelfu ya spishi za mimea na wanyama zimeathirika na kutoweka kutokana na uharibifu wa makazi, uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa. Uharibifu wa spishi yoyote huibua msururu wa matokeo hasi katika mfumo ikolojia na hivyo kuvuruga uwiano wa kimazingira.
Matokeo ya tatu ni kuongezeka migogoro ya kijamii na kiuchumi. Uharibifu wa mazingira unaweza kusababisha uhamaji mkubwa, migogoro ya rasilimali za maji na chakula na kuongeza umaskini. Maeneo mengi ya dunia yanakabiliwa na migogoro ya kibinadamu kutokana na ukame au uchafuzi wa maji.
Kwa ujumla, ubepari hauwezi kuendana na mazingira bila kufanyiwa mageuzi ya kimuundo. Unyonyaji wa maliasili utaendelea tu maadamu faida inapewa kipaumbele juu ya usalama wa dunia na wanadamu. Suluhisho linapatikana katika kubadili mifumo ya uzalishaji, upunguzaji matumizi, kuimarisha sheria za mazingira na kuelekea upande wa uchumi endelevu, ambao unazingatia maliasilia si kama rasilimali isiyoisha, bali kama urithi wa pamoja na wa kiwango maalum kwa ajili ya wanadamu wote.