Kwa nini watawala wa Marekani wanajaribu kujitenga na chokochoko za Netanyahu?
Kushirikiana kwa utawala wa Trump na vitendo vya jinai na uchokozi vya Israel katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumekuwa na taathira mbaya kwa msimamo wa serikali ya sasa ya Marekani mbele ya maoni ya umma ndani na nje ya nchi hiyo.
Huku wananchi wa Marekani wakiendelea kukasirishwa na vita vya kichokozi vya nchi hiyo pamoja na utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran, viongozi wa ngazi za juu wa Washington sasa wanajaribu kujitenga na chokochoko za Israel katika eneo. Katika msimamo wa karibuni kuhusu suala hili, JD Vance Makamu wa Rais wa Marekani amedai kwamba baadhi ya wakati, malengo ya Marekani hutofautiana na ya Israel kuhusu Iran na kwamba Washington inataka tu Iran isipate silaha za nyuklia.
Rais Donald Trump wa Marekani awali alisisitiza kuwa yeye ndiye anayefanya maamuzi ya mwisho kuhusu vita na Iran na kwamba Benjamin Netanyahu lazima afuate maamuzi ya rais wa Marekani kuhusiana na suala hilo.
Hii ni katika hali ambayo siku zote, watawala wa Marekani, hasa kutoka chama cha Republican, wamekuwa wakidai kwamba wanaunga mkono kikamilifu sera za Israel na kwamba hakuna tofauti zozote zilizopo kati ya Washington na Tel Aviv katika uwanja huo. Kwa mfano, Trump amekuwa akisema mara kwa mara kwamba hakuna rais yeyote wa Marekani ambaye ameunga mkono Israel kama anavyofanya yeye na kwamba katika kipindi cha utawala wake, ushirikiano wa hali ya juu umeanzishwa kati ya Marekani na Israel. Netanyahu pia amesisitiza mara kwa mara kwamba Israel haijawahi kuwa na rafiki mzuri kama Trump katika Ikulu ya White House.
Hata hivyo, kujihusisha utawala wa Trump katika vitendo vya jinai na uchokozi wa Israel katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumekuwa na taathira kubwa katika msimamo wa serikali ya sasa ya Marekani mbele ya maoni ya waliowengi ndani na nje ya nchi hiyo. Hivi sasa, matokeo ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kudhibitiwa safari za meli katika Lango-Bahari la Hormuz, yameweka mzigo mkubwa katika maisha ya Wamarekani. Vita hivi vimeongeza kwa kiasi kikubwa bei ya nishati, ikiwa ni pamoja na petroli, huko Marekani na hivyo kuongeza mfumuko wa bei nchini. Aidha askari wengi wa Marekani wameuawa katika vita hivi, ambapo uharibifu wa makumi ya mabilioni ya dola umesababishwa katika uchumi wa nchi kutokana na gharama za vita na mashambulizi ya Iran dhidi ya mali ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Hali hii imepelekea Trump kutuhumiwa kuwa hana busara na kwamba amefanya makossa makubwa katika kuanzisha vita visivyo na udharura wowote dhidi ya Iran; vita ambavyo kimsingi vinatumikia maslahi ya Israel na sio ya Marekani.
Sasa Wamarekani wengi wanaamini kuwa Netanyahu ndiye aliyemburuza Trump kwenye vita hivi visivyo na tija na ghali mno kwa Wamarekani na kwamba Trump amekanyaga waziwazi kauli mbiu yake mwenyewe ya eti “Marekani Kwanza” ili kuwafurahisha Wazayuni.
Katika anga hiyo, Trump na Vance sasa wanajaribu kubadilisha taswira hii mbaya mbele ya maoni ya umma ndani na nje ya Marekani na kuidhihirisha Washington kuwa huru mkabala wa mienendo na matakwa ya Wazayuni. Bila shaka, kama msimamo wa Israel ungekuwa mzuri mbele ya maoni ya umma duniani, ikiwemo nchini Marekani, watawala wa serikali ya Marekani hawangelazimika kujiweka katika hali ngumu ya kujaribu kujitenga na uchokozi pamoja na jinai za Wazayuni. Wanatumai kwamba kupitia tiba ya mazungumzo, wataweza kujiondolea katika unyanyapaa wa kufuata jinai na uchochezi wa Wazayuni. Hata hivyo, madai hayo, kwa kuzingatia historia ya Washington ya uungaji mkono usioyumba kwa Tel Aviv, hususan misimamo ya Trump na utawala wake ya kutoa uungaji mkono usio na masharti kwa Netanyahu, yamepunguza sana ukweli wa madai yenyewe, na ndio maana sasa Trump na Vance wanatapatapa na kuzungumza na vyombo vya habari mara kwa mara ili kujaribu kujiondolea lawama ya kushirikiana na Wazayuni katika uchokozi wao dhidi ya nchi za eneo, kwa madhara ya walipakodi wa Marekani.