Iran yaongoza miongoni mwa nchi bora duniani katika Mikroelektroniki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139042-iran_yaongoza_miongoni_mwa_nchi_bora_duniani_katika_mikroelektroniki
Iran imejitokeza kama taifa linaloongoza kwa uzalishaji wa kisayansi katika nyanja ya mikroelektroniki miongoni mwa nchi za Kiislamu, huku ikishika nafasi ya kwanza katika matawi mengi muhimu ya sekta hiyo na kupanda hadi kuwa miongoni mwa mataifa 16 bora duniani katika uwezo wa kisayansi wa sekta hiyo.
(last modified 2026-06-11T03:12:39+00:00 )
Jun 11, 2026 03:09 UTC
  • Iran yaongoza miongoni mwa nchi bora dunani katika Mikroelektroniki
    Iran yaongoza miongoni mwa nchi bora dunani katika Mikroelektroniki

Iran imejitokeza kama taifa linaloongoza kwa uzalishaji wa kisayansi katika nyanja ya mikroelektroniki miongoni mwa nchi za Kiislamu, huku ikishika nafasi ya kwanza katika matawi mengi muhimu ya sekta hiyo na kupanda hadi kuwa miongoni mwa mataifa 16 bora duniani katika uwezo wa kisayansi wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni zilizotolewa na Taasisi ya Nukuu na Ufuatiliaji wa Sayansi ya Ulimwengu wa Kiislamu (ISC), Iran inashika nafasi ya kwanza kati ya nchi 57 za Kiislamu katika matawi matano kati ya sita makuu ya teknolojia ya mikroelektroniki.

Ripoti hiyo imesema kuwa, katika kiwango cha dunia, Iran kwa sasa inashika nafasi kati ya ya 12 na ya 16 kwa uzalishaji wa kisayansi katika nyanja hiyo.

Teknolojia ya mikroelektroniki inajumuisha maeneo mbalimbali ya kitaalamu, yakiwemo saketi jumuishi, vifaa vya semikondakta, vipengele vya superkondakta, vipengele vinavyotokana na polima, vifaa chipukizi, pamoja na mifumo midogo ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Iran imeonyesha uwezo mkubwa hasa katika teknolojia za hali ya juu na zile zinazoibuka kwa kasi.

Katika eneo la vipengele vya kielektroniki vinavyoibuka pekee, ambalo linachukuliwa kuwa miongoni mwa matawi ya kisasa zaidi na yanayokua kwa haraka katika mikroelektroniki , watafiti wa Iran wamechapisha takribani makala 5,000 za kisayansi katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Rais wa ISC, Mohammad Mehdi Alavian-Mehr, amesema kuwa kasi ya ukuaji wa kisayansi wa Iran katika mikroelektroniki ni matokeo ya miongo kadhaa ya uwekezaji endelevu katika utafiti na maendeleo ya kitaaluma.

Aidha, amebainisha kuwa machapisho ya kisayansi ya Iran yaliyosajiliwa katika fahirisi za kimataifa yameshuhudia ongezeko kubwa mno katika kipindi cha miaka 40 iliyopita.

Amesema: “Mwaka 1980, Iran ilikuwa na takribani machapisho 300 tu yaliyosajiliwa katika kanzidata za kimataifa za kisayansi, lakini sasa idadi hiyo imefikia karibu 80,000.”

Tangazo hilo pia limekuja sambamba na dalili pana zaidi za kuongezeka kwa ushawishi wa kisayansi wa Iran katika medani ya kimataifa.

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizochapishwa na ISC, Iran kwa sasa inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa wazalishaji 20 wakubwa wa sayansi duniani kwa ufanisi wa uchapishaji, ikizalisha machapisho mengi zaidi ya kisayansi yaliyofahirisiwa kimataifa kwa kila dola ya utafiti kuliko taifa jingine lolote kubwa la kisayansi.