Je, siasa zinapoingizwa michezoni, FIFA bado huwa ndiyo inayochukua maamuzi?
Kombe la Dunia la mchezo wa kandanda, ambalo waasisi wake wamekuwa wakidai kuheshimu maadili na thamani za kimataifa pamoja na kutenganishwa siasa na mchezo huo, sasa limekuwa mateka wa siasa za mabavu na ubaguzi wa serikali ya Marekani, ambapo hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lenyewe limeshindwa kutetea na kuwalinda maafisa wake mbele ya siasa hizo.
Michuano ya Kombe la Dunia inaanza rasmi siku ya Alhamisi, ikiandaliwa na nchi tatu za Marekani, Mexico na Canada. Hata hivyo, kombe hilo sasa limeathiriwa pakubwa na sera za uhamiaji za serikali ya Marekani. Kombe la Dunia ni tukio muhimu la kimataifa ambapo wachezaji bora, makocha, waamuzi, waandishi wa habari na mashabiki kutoka pembe zote za dunia hukusanyika kwa ajili ya kushuhudia pamoja na kufurahia tukio hilo la michezo. Serikali ya Marekani, ambayo ndiyo mwenyeji mkuu wa Kombe la Dunia la 2026, imedhoofisha pakubwa itibari ya tukio hilo ambalo linatakiwa kutengwa na masuala ya kisiasa, kwa kutekeleza sheria za kibaguzi za uhamiaji na usalama dhidi ya baadhi ya washiriki.
Katika hatua ya karibuni, serikali ya Marekani imemnyima kibali cha kuingia nchini humo Omar Artan, mwamuzi wa kimataifa kutoka Somalia na refa mashuhuri barani Afrika, na hatimaye kuamuru arudishwe nchini kwake baada ya kuhojiwa na kudhalilishwa kwa saa 11 na maafisa wa uhamiaji wa Marekani. Mnamo Juni 2025, Trump alipiga marufuku kuingia Marekani raia wa nchi 12, zikiwemo Somalia, Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Iran na Haiti. Pia aliwaita wahamiaji wa Somalia "takataka" kabla ya droo ya Kombe la Dunia mnamo Desemba 2025 na kusema wanapaswa "kurudi walikotoka." La kusikitisha zaidi ni kwamba, FIFA ilitoa taarifa bila kupinga hatua hiyo ya kibaguzi ya serikali ya Marekani, ikidai: "FIFA haihusiki na mchakato wa uhamiaji wa nchi mwenyeji, ikiwa ni pamoja na utoaji wa visa, na kuwa FIFA imefahamishwa na maafisa wa Marekani kwamba hali ya Artan haitabadilishwa kwa sasa." Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza na Arsenal Ian Wright ameandika katika mtandao wa kijamii kwamba: "Kila baada ya saa chache, hutokea kisa kipya: Shabiki kukataliwa, mchezaji kukataliwa, afisa kukataliwa, ripota kukataliwa, na sasa mwamuzi. Hili ni Kombe la Dunia lenye vurugu na kuchanganyikiwa."
Huu si mfano pekee wa namna serikali ya Marekani inavyotumia kisiasa Kombe la Dunia na hivyo kuzuia kufanyika michuano ya mchezo huu kwa njia ya haki. Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni alitamka wazi kuwa ingekuwa bora kwa timu ya taifa ya Iran kutoenda Marekani, kwa ajili ya kulinda usalama wake. Wakati huo huo, serikali ya Marekani pia imezuia na kuvuruga mchakato wa kupewa viza timu ya taifa ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa upande mmoja, kwa kuchelewesha utoaji visa kwa timu hii, timu ya taifa ya kandanda ya Iran imelazimika kukaa nchini Mexico, licha ya kuwa inapasa kuchezea michezo yake huko Marekani. Kwa upande mwingine, imewapa wachezaji wa timu ya Iran visa ya masaa machache tu kuwa Marekani, ambapo wanatakiwa kurejea Mexico punde baada ya kumalizika michezo waliyopangiwa, jambo ambalo ni kinyume na sheria za FIFA na linalenga kutoa mashinikizo yasiyo ya kawaida dhidi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Iran. Ingawa FIFA haijaonyesha upinzani wowote dhidi ya siasa na mienendo hiyo ya kibaguzi ya serikali ya Marekani, lakini kuna matukio mengi huko nyuma ambayo yaliamsha hasira ya FIFA na kuipelekea kupiga marufuku ushiriki wa baadhi ya nchi au kuzinyima fursa ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia. Russia iliondolewa na FIFA kwenye mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la 2022 kutokana na vita vyake nchini Ukraine. Mwaka 2023, FIFA iliipokonya Indonesia fursa ya kuandaa Kombe la Dunia la U-20 baada ya viongozi wa kieneo wa nchi hiyo kukataa kuiruhusu Israel ishiriki.
Lakini sasa FIFA hiyo hiyo inajifanya kutokuwa na uwezo wa kufanya lolote katika kukabiliana na ubaguzi wa utawala wa Marekani katika maandalizi ya Kombe la Dunia. Baadhi ya wajuzi wa mambo wanaamini, kwamba uhusiano mkubwa wa Gianni Infantino, Mkuu wa FIFA na Rais Donald Trump wa Marekani, ndio umepelekea FIFA kufumbia macho ukandamizaji na siasa hizo za kibaguzi za Marekani katika michezo ya Kombe la Dunia. Siasa katika Kombe la Dunia hazionekani tu katika kauli mbiu au hotuba, bali zimedhihiri wazi katika kiwango cha utekelezaji, ambapo Kombe la Dunia sio tena mashindano ya michezo tu, bali ni hatua ya kutumia nguvu ya serikali dhidi ya pande zisizohitajika. FIFA imekuwa mateka wa siasa za undumakuwili wa kimataifa, ambapo nchi moja kama Indonesia inanyimwa fursa ya kuanda michezo ya Kombe la Dunia na nyingine kama Marekani inapewa fursa hiyo kwa mikono miwili licha ya kukiuka wazi wazi maadili na sheria za FIFA, kwa sababu tu ina misuli na nguvu za kufanya hivyo. Hali inasikitisha zaidi tunapotilia maanani kwamba nchi kama hiyo inayotumia mabavu, kudhalilisha na kubagua hadharani baadhi ya washiriki wa michezo ya Kombe la Dunia, rais wake anapewa eti Tuzo ya Amani, tena na Infantino mwenyewe, Mkuu wa FIFA. Rais huyo ambaye mikono yake imetapakaa damu ya watu wa Gaza, Lebanon, Yemen na Iran na ambaye amepokea eti Tuzo ya Amani kutoka kwa rais wa FIFA, sasa ameitwisha FIFA yenyewe siasa zake za mabavu na hivyo kutilia shaka itibari na uhuru wake wa maamuzi.