DA yakanusha madai ya Trump ya kuwepo mauaji ya Wazungu A/Kusini
Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini (DA), John Steenhuisen amekadhibisha madai ya kuwepo "mauaji ya kimbari ya Wazungu" nchini Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa DA amesema hakuna "mauaji ya kimbari ya Wazungu" nchini Afrika Kusini, bali kinachoshuhudiwa ni tatizo kubwa na pana la uhalifu linaloathiri raia wote bila kujali rangi na asili zao.
Amesema: Takwimu rasmi zinaonyesha wazi kabisa tatizo la uhalifu liko wapi, na ni nani anayebeba mzigo huo, si mauaji ya kimbari ya Wazungu, hata kidogo."
Steenhuisen amefafanua kwa kusema, "Tuna wazungu waliouawa, ndiyo. Lakini pia tuna Waafrika Kusini weusi, pamoja na Waafrika Kusini Wahindi na watu wengine wa asili ya Asia Kusini ambao pia wanauawa."
Matamshi ya kiongozi huyo wa DA yametolewa kujibu madai ya kukaririwa ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye hivi karibuni aliliambia Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos kwamba, Afrika Kusini inashuhudia "mauaji ya kimbari ya Wazungu" na kukosoa jinsi jamii za Waafrikana eti zinavyonyanyaswa.
Kiongozi huyo wa chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini amesema kwamba, Trump alikuwa akiendeleza simulizi inayoendana na ajenda yake mwenyewe, bila kujali ukweli na uhalisia wa mambo.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, tuhuma zizisizo na mashiko za "mauaji ya Wazungu" huko Afrika Kusini ni mojawapo ya madai yanayoenezwa na Trump kwa ajili ya kuamsha hisia za makundi ya ubaguzi wa rangi na yenye misimamo ya kufurutu ada duniani.