Africa CDC yatoa tahadhari kufuatia mlipuko wa Ebola Kongo kushindwa kudhibitiwa
-
Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Jean Kaseya
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika ( AFRICA CDC) kimetahadharisha kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unazidi kuwa nje ya udhibiti, huku vifo zaidi ya 1,700 vikirekodiwa ndani ya wiki 14 pekee. Hii ni katika hali ambayo juhudi za kuwafuatilia watu waliotangamana na wagonjwa zimeshindwa kudhibiti msambao wa virusi hivyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Jean Kaseya, amesema kuwa hatua za kukabiliana na kudhibiti kasi ya maambukizo ya Ebola ni za kiwango cha chini na ametahadharisha kuwa ufuatiliaji wa watu waliotangamana na wagonjwa haujawa na matunda ya kuridhisha.
Akizungumza katika ziara yake katika mji wa Bunia jana Jumanne, Kaseya alisema karibu asilimia 70 ya maambukizi mapya yalikuwa yakitokea nje ya orodha zinazojulikana za watu waliotangamana na wagonjwa; hali inayoashiria kuenea kwa maambukizi katika jamii na hivyo amesisitiza umuhimu kuandaliwa mkakati mpya.
Watu 3,802 wameambukizwa na wengine 1,707 wamepoteza maisha kutokana na Ebola tangu kutangazwa mlipuko wa ugonjwa huo tarehe 15 Mei, na hivyo kuufanya kuwa mlipuko wa Ebola unaoenea kwa kasi zaidi kuwahi kusajiliwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (AFRICA CDC) amesema kuwa mlipuko wa sasa wa Ebola ulioikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni wa pili kwa ukubwa duniani; ambapo baada ya wiki mbili tu mlipuko huo ulikuwa umeenea pakubwa mara saba zaidi ya mlipuko wa Ebola ulioiathiri Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2016.
Jan Kaseya Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC na mwenzake wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, jana walliutembelea mji wa Bunia kwa lengo la kuzindua kituo kipya cha matibabu ya Ebola.
Dakta Janabi amesema kuwa upimaji wa maabara wa kila siku umeongezeka kutoka sampuli zipatazo 30 hadi zaidi ya 2,000, huku uwezo wa kutoa matibabu ukiongezeka kufikia takriban vitanda 1,000. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa bado hazitoshi, kwa kuwa watu wanaendelea kupoteza maisha.