Save the Children: Sudan inapitia kipindi kirefu zaidi cha kufungwa shule duniani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135790-save_the_children_sudan_inapitia_kipindi_kirefu_zaidi_cha_kufungwa_shule_duniani
Shirika la Save the Children limeonya kwamba vita vinavyoendelea nchini Sudan vimewanyima elimu watoto zaidi ya milioni 8, katika kile kinachoelezwa kama kipindi kirefu zaidi cha kufungwa shule duniani.
(last modified 2026-01-23T03:22:33+00:00 )
Jan 23, 2026 03:22 UTC
  • Save the Children: Sudan inapitia kipindi kirefu zaidi cha kufungwa shule duniani
    Save the Children: Sudan inapitia kipindi kirefu zaidi cha kufungwa shule duniani

Shirika la Save the Children limeonya kwamba vita vinavyoendelea nchini Sudan vimewanyima elimu watoto zaidi ya milioni 8, katika kile kinachoelezwa kama kipindi kirefu zaidi cha kufungwa shule duniani.

Shirika hilo limesema katika taarifa yake kwamba zaidi ya watoto milioni 8, ambao ni karibu nusu ya watoto wa umri wa kwenda shule, wametumia siku 484 bila kuhudhuria darasa lolote, likisisitiza kwamba kipindi hiki kinazidi hata vipindi vya karantini na kufungwa shughuli zote ambavyo dunia ulipitia wakati wa janga la COVID-19.

Sudan inasumbuliwa na vita vya ndani vinavyoendelea tangu 2023 kati ya jeshi la taifa na waasi wa Rapid Support Forces (RSF), ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya raia kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. Vita hivyo pia vimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, haswa katika sekta za afya na elimu.

Kwa mujibu wa Save the Children, Sudan inakabiliwa na mojawapo ya migogoro mibaya zaidi ya elimu duniani, huku idadi kubwa ya shule zikiwa zimefungwa kabisa, na zingine zikiwa zimeharibiwa au kugeuzwa kuwa makazi ya watu waliokimbia makazi yao.

Save the Children: Watoto milioni 8 hawaendi shule Sudan

Jimbo la Darfur, ambalo sehemu yake kubwa inadhibitiwa na RSF, ndilo lililoathiriwa zaidi, likiwa na 3% pekee ya shule zinazofanya kazi kati ya shule zote zaidi ya 1,100 za jimbo hilo.

Oktoba mwaka jana, waasi wa Rapid Support Forces (RSF), walitwaa El Fasher, mji mkuu wa jimbo hilo, na hivyo kuimarisha udhibiti wao katika eneo hilo.

Taarifa ya  Save the Children inaonyesha kuwa idadi kubwa ya walimu wamelazimika kuacha kazi zao kutokana na kusimamishwa malipo ya mishahara, jambo lililozidisha kuporomoka sekta ya elimu nchini Sudan.

Mkurugenzi Mtendaji wa Save the Children, Inger Ashing, ameonya kwamba kushindwa kuwekeza katika elimu "kutakifanya kizazi kizima kinaswe katika mustakabali unaotawaliwa na migogoro."