Ripoti: Zaidi ya raia 370 waliuawa Kivu, mwezi Desemba 2025
-
Ripoti: Zaidi ya raia 370 waliuawa Kivu, mwezi Desemba 2025
Imeelezwa kuwa, zaidi ya raia 370 waliuawa Kivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi Disemba mwaka jana.
Katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mwezi Desemba 2025 ulikuwa mwezi hatari sana, kulingana na Kipimo cha Usalama cha Kivu. Zaidi ya waathiriwa 370 wa kiraia walirekodiwa na programu hii, ambayo imekuwa ikirekodi matukio mashariki mwa nchi tangu mwaka 2017. Baada ya miezi kadhaa ya kukatizwa, shirika hili lilianza tena ukusanyaji wake wa data, na kuzorota kwa usalama kumeshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni.
Mwezi huu Desemba 2025 ulikuwa mwezi mbaya zaidi huko Kivu, kulingana na ripoti hii. Mwelekeo huu unatumika tu kwa miezi michache iliyopita kwa sababu, kufuatia kutekwa kwa mji wa Goma na Bukavu, Kipimo cha Usalama cha Kivu kililazimika kusitsha kazi yake na kujipanga upya.
Takwimu hizi mpya zinatuambia kwamba hali ya usalama mashariki mwa DRC haiboreki hata kidogo: raia 379 waliuawa - na hii inajumuisha waathiriwa waliorekodiwa tu - raia 129 walitekwa nyara, matukio 274 ya usalama, na mapigano 141 yalirekodiwa. Karibu takwimu hizi zote zimeongezeka.
Vifo vingi vilirekodiwa katika mkoa wa Kivu Kusini. Hii inaambatana na shambulio jipya lililoanzishwa mapema mwezi Desemba na kundi lenye silaha la AFC/M23, linaloungwa mkono na vikosi vya Rwanda, katika jiji la Uvira.
Ripoti hii pia inaonyesha hali inayozidi kuwa mbaya huko Ituri, mkoa ulioko kaskazini zaidi. Shirika hili linataja tukio kubwa ambalo lilihusisha jeshi la Kongo dhidi ya mshirika wake wa Uganda, UPDF, katika eneo la Djugu mapema mwezi Desemba, na mapigano kati ya wanajeshi ambayo yalisababisha vifo kadhaa.