Umoja wa Afrika waiondolea vikwazo Guinea
-
Umoja wa Afrika waiondolea vikwazo Guinea
Umoja wa Afrika umetangaza kuiondolea vikwazo Guinea ilivyoiwekea kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021, baada ya nchi hiyo kuandaa uchaguzi wa rais mwezi Disemba.
Taarifa ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika imesema kuwa, Guinea imepiga hatua katika utekelezaji wa mkakati wa kipindi cha mpito ambacho kiliishia kwa kuandaliwa kwa uchaguzi wa mwezi uliopita.
Umoja huo wa Afrika umempongeza kiongozi wa zamani wa jeshi Mamady Doumbouya kwa kuchaguliwa kwake. Doumbouya aliapishwa kama rais Jumamosi iliyopita mbele ya maelfu ya wafuasi wake na marais kadhaa.
Doumbouya alimpindua rais Alpha Conde mwaka 2021 na tangu aingie madarakani alibinya uhuru wa kiraia na kupiga marufuku maandamano.
Wapinzani wake wa kisiasa wamekamatwa, kufunguliwa mashtaka au kukimbilia uhamishoni.
Uchaguzi huo wa Disemba mwaka jana ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini humo tangu Doumbouya alipompindua Rais Alpha Conde miaka minne iliyopita.
Doumbouya aliapishwa rasmi Jumamosi iliyopita kuwa Rais wa Jamhuri ya Guinea baada ya kuibuka na ushindi wa asilimia 86.72 ya kura katika uchaguzi wa Rais wa Disemba 28 nchini humo na hivyo kuashiria kurejea Guinea katika utawala wa katiba kufuatia kipindi cha mpito cha uongozi wa kijeshi wa zaidi ya miaka minne.
Mamady Doumbouya ataiongoza Guinea kwa muhula wa miaka saba. Kwa mujibu wa Kifungu cha 59 cha Katiba ya Guinea, Doumbouya alikula kiapo mbele ya Mahakama ya Juu, iliyoongozwa na rais wake wa kwanza, Fode Bangoura, ambapo amaeahidi kuwa muaminifu kwa taifa hilo na kuheshimu utawala wa sheria.