CDC: Mlipuko wa Mpox barani Afrika sio dharura tena ya kiafya
-
CDC: Mlipuko wa Mpox barani Afrika sio dharura tena ya kiafya
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (CDC) ametangaza kuwa, mlipuko wa Mpox barani Afrika kwa sasa sio "dharura ya kiafya barani humo.
Jean Kaseya akitangaza uamuzi huo amesifu ubora wa mwitikio ulioratibiwa kwa ugonjwa huo, ambao unaweza kutumika kama mfano wa siku zijazo.
Hali ya dharura ilitangazwa mnamo mwezi Agosti 2024. Kufikia mwisho wa mwaka huo, zaidi ya watu 80,000 waliambukizwa virusi vya Mpox na watu 1,340 kufariki dunia huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikihusika karibu katika visa vyote.
Mwaka mmoja na nusu baadaye, hali hii ya dharura imeondolewa.
Katika kipindi hicho, zaidi ya dola bilioni moja zilitengwa, mifumo ya ufuatiliaji na uchunguzi iliboreshwa sana, na dozi milioni 5 za chanjo zilisambazwa katika nchi 16. Kufikia mwisho wa mwaka 2025, idadi ya visa vilivyothibitishwa ilipungua kwa 60%, na kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa huo kilipungua kutoka 2.6% hadi 0.6%.
Taarifa zaidi zinasema, mafanikio haya yanakaribishwa na CDC Afrika, ambayo iliratibu juhudi hii. Hata hivyo, Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vinasisitiza kwamba, tangazo hili halimaanishi kwamba virusi havisambai tena: vinabaki kuwa vya kawaida katika maeneo kadhaa. Hata hivyo, zana sasa zipo ili kuhama kutoka kwa mwitikio wa dharura hadi awamu endelevu ya kuzuia na kudhibiti, inayoongozwa na nchi zenyewe.
CDC inaongeza kuwa mfumo huu wa usimamizi sasa utatumika kama mfano kwa magonjwa mengine yenye uwezekano wa mlipuko, kama vile Kipindupindu, Dondakoo, Surua, na Polio.