Tovuti ya Israel: Ujerumani inaendelea kufadhili mauaji ya kimbari huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135788-tovuti_ya_israel_ujerumani_inaendelea_kufadhili_mauaji_ya_kimbari_huko_gaza
Tovuti ya Israel, 972+ imechapisha ripoti ndefu ya uchunguzi kuhusu uhusiano wa kijeshi kati ya Ujerumani na Israel, ikihitimisha kwamba mauzo ya silaha ya Ujerumani yameendelea kumiminika Israel licha ya madai kwamba yamesitishwa kutokana na mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza.
(last modified 2026-01-23T03:22:02+00:00 )
Jan 23, 2026 03:22 UTC
  • Tovuti ya Israel: Ujerumani inaendelea kufadhili mauaji ya kimbari huko Gaza
    Tovuti ya Israel: Ujerumani inaendelea kufadhili mauaji ya kimbari huko Gaza

Tovuti ya Israel, 972+ imechapisha ripoti ndefu ya uchunguzi kuhusu uhusiano wa kijeshi kati ya Ujerumani na Israel, ikihitimisha kwamba mauzo ya silaha ya Ujerumani yameendelea kumiminika Israel licha ya madai kwamba yamesitishwa kutokana na mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza.

Ripoti hiyo, iliyoandaliwa na mwandishi Hanno Hauenstein, imeelezea kwamba Ujerumani imevuka mipaka ya kisheria katika kutuma silaha huko Israel, na kwamba haikuacha kutoa silaha kwa Israel kwa ajili mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza, bali ilifanya makubaliano mapya ya pande mbili ya usalama wa mtandao na kuendelea kutuma silaha.

Ripoti ya Hauenstein imesema kwamba matukio ya hivi karibuni katika uhusiano wa Ujerumani na Israel yamefichua mabadiliko makubwa ambayo yanazidi msaada wa kidiplomasia hadi ushirikiano wa kina wa kijeshi na kiusalama, ambao duru za haki za binadamu zimeuelezea kuwa unachangia moja kwa moja katika mauaji ya kimbari ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Hauenstein ameeleza kuwa Ujerumani ilitangaza mnamo Agosti 2025 kwamba inasimamisha baadhi ya vibali vya usafirishaji wa silaha kwenda Israel kwa ajili ya vita vya Gaza kutokana na mashinikizo yaliyosababishwa na picha za mauaji ya kimbari kutoka Ukanda wa Gaza na mabadiliko ya maoni ya umma. Hata hivyo, anasema Hauenstein, Ujerumani iliidhinisha tena utumaji wa silaha huko Israel mara tu baada ya kusitishwa mapigano Oktoba 2025, akithibitisha kwamba kusitishwa huko kulikuwa mbinu ya kutuliza hasira za umma na sio mabadiliko ya mkakati.

Ripoti ya Hanno Hauenstein inasisitiza kuwa mauaji ya kimbari sasa hayatambuliwi tena kauwa ni uhalifu wa kimataifa, bali ni uhalifu kwa masharti, ambao hupuuzwa au kuruhusiwa unapofanywa na mshirika wa nchi za Magharibi.

Maelfu ya watoto wameuawa katika mauaji ya kimbari ya Israel

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Palestina imeeleza katika takwimu zake za hivi karibuni kwamba, Wapalestina zaidi ya 71,000 wameuawa shahidi katika vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, Oktoba 2023.