Madaktari Sudan watahadharisha kuhusu maafa tarajiwa ya kibinadamu huko Kordofan Kusini
-
Wakimbizi Kordofan Kusini
Kundi la madakatri wa Sudan limetahadharisha kuhusu maafa tarajiwa ya kiafya na kibinadamu katika mji wa Dalang unaopatikana katika jimbo la Kordofan Kusini. Kundi hilo limesema kuwa mji wa Dalang unaendelea kuzingirwa huku ukikabiliwa na mashambulizi makali ya wanagambo wa RFS.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan ambayo ni taasisi isiyo ya kiserikali umeeleza kuwa mashambulizi makali ya mabomu katika mji wa Dalang yanajiri kila siku, na hadi sasa watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema umeshindwa kukusanya takwimu sahihi kwa sababu mawasiliano ndani ya mji huo yamekatwa huku vituo vya afya vikikumbwa na uhaba wa chakula na suhula muhimu za matibabu.
Mtandao huo umeyatolea mwito mashirika ya masuala ya kiinadamu na taasisi za kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuhitimisha mzingiro katika mji wa Dalang, kuhakikisha chakula na misaada ya dawa inafika katika mji huo na kuwalinda raia na wafanyakazi wa sekta ya afya.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan pia umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua mara moja ili kuiepusha Kordofan Kusini na senario sawa na ile iliyoshuhudiwa katika mji wa Al Fasher ulioangukia mikononi mwa wanamgambo wa RSF Oktoba 26 mwaka jana.
Taasisi za ndani za kimataifa zimeripoti kuuawa kwa halaiki raia katika mji huo.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, miji ya Dalang na Kadugli imezingirwa na wanamgambo wa RSF na harakati ya SPLM-N tangu miezi ya awali ya kuanza vita yapata zaidi ya miaka miwili sasa.