Marufuku ya kuingia wanariadha wa utawala wa Kizayuni nchini Indonesia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i132458-marufuku_ya_kuingia_wanariadha_wa_utawala_wa_kizayuni_nchini_indonesia
Indonesia inachukulia marufuku ya kuingia wanariadha wa utawala Kizayuni wa Israel katika nchi hiyo kuwa haki yake halali.
(last modified 2025-10-27T05:42:34+00:00 )
Oct 27, 2025 04:30 UTC
  • Marufuku ya kuingia wanariadha wa utawala wa Kizayuni nchini Indonesia

Indonesia inachukulia marufuku ya kuingia wanariadha wa utawala Kizayuni wa Israel katika nchi hiyo kuwa haki yake halali.

Indonesia imepiga marufuku kuingia kwa wanariadha wa Israel katika nchi hiyo kwa msingi wa siasa za kuunga mkono Palestina na maslahi ya umma. Uamuzi huu umekabiliwa na hisia tofauti za kimataifa, lakini serikali ya Jakarta inaendelea kusisitiza msimamo wake huo. Indonesia imekabiliwa na vitisho kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki baada ya kufutilia mbali viza za wanachama wa timu ya Israel waliokusudia kushiriki Mashindano ya Dunia ya Gymnastics mjini Jakarta, lakini maafisa wa Jakarta wanasisitiza kuwa uamuzi huo umechukuliwa ili kulinda "usalama na maslahi ya umma".

Eric Tohir, Waziri wa Michezo na Vijana wa Indonesia, amesema katika muktadha huu kwamba uamuzi wa nchi hiyo umechukuliwa kwa mujibu wa sheria za sasa na katiba ya nchi ya 1945, ambayo inaipa serikali jukumu la kusaidia "kudumisha utulivu wa umma". Ameongeza kuwa Indonesia inafuata "kanuni ya kudumisha usalama, utulivu na maslahi ya umma katika tukio lolote la kimataifa" na hivyo kuzuiwa wajumbe wa Israel kushiriki mashindano hayo kumetimia kwa msingi huo.

Serikali ya Indonesia imesema kwamba itashikilia uamuzi wake wa kuwanyima visa wanariadha wa Israel kwa ajili ya Mashindano ya Dunia ya Gymnastics, ambayo yamepangwa kufanyika nchini kuanzia Novemba 19 hadi 25, ingawa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imeonya kuwa itasitisha kwa muda kufanyika nchini humo mashindano ya kimataifa ikiwa marufuku hiyo itaendelea kutekelezwa. Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa ilitangaza katika taarifa yake kuwa itashauri mashirikisho ya kimataifa kutoandaa hafla au mikutano ya kimataifa nchini Indonesia hadi ihakikishe ushiriki wa washiriki wote bila kujali utaifa wao. Wakati huo huo, Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imekataa ombi la Israel la kushiriki mashindano hayo na kuunga mkono uamuzi wa Indonesia.

Uamuzi huo umechukuliwa ikiwa ni katika kujibu hatua za kijeshi za Israel huko Gaza na "mauaji ya kimbari" ya watu wa Gaza, na ikiwa ni sehemu ya sera ya msingi ya nchi hii ya kuwatetea watu wa Palestina.

Upinzani wa kushirikishwa Utawala wa Kizayuni katika michezo ya kimataifa

Hatua hii ya Indonesia inajiri huku baadhi ya wachambuzi wakiikosoa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kwa kutekeleza siasa za "undumakuwili". Kwa mfano, baada ya kuanza vita vya Russia na Ukraine mnamo Februari 2022, kamati hiyo ilipiga marufuku Russia kushiriki michezo ya Olimpiki ya Paris ya 2024, lakini wakati huo huo, ikawaruhusu wanariadha wengine wa Russia kushiriki kama wasiounga mkono upande wowote. Wanamichezo wa utawala wa Kizayuni waliruhusiwa kushiriki katika michezo hiyo ya Paris wakiwa wanapeperusha bendera ya utawala huo, huku maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza yakishambuliwa vikali na jeshi la utawala wa Kizayuni. Maafisa wa Palestina wanasema tangu kuanza mashambulizi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, zaidi ya wanariadha 800 wameuawa shahidi huko Gaza, na miundombinu ya michezo, pamoja na usambazaji wa chakula na vifaa vya matibabu, vimeharibiwa katika sehemu zote za ukanda huo.

Huku hatua hii ya Indonesia ikiwiana kikamilifu na sera za kigeni za nchi hii katika kuulaani utawala wa Kizayuni na kuendana na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa kadhia ya Palestina, hiyo ni taswira tosha ya harakati ya kimataifa ya kuwaunga mkono Wapalestina na kuzidi kutengwa utawala wa Kizayuni kimataifa, ikiwemo katika medani ya michezo.

Kutengwa Israel katika michezo kunazidi kushika kasi kufuatia matukio ya kisiasa na radiamali ya nchi tofauti kuhusiana na hatua za utawala huo ghasibu hasa huko Palestina, na hicho ni kielelezo cha kutengwa kisiasa utawala huo katika ngazi za kimataifa. Katika miaka ya hivi karibuni, hasa kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza, baadhi ya nchi zikiwemo Indonesia na Malaysia zimepiga marufuku wanariadha wa Israel kuingia katika ardhi zao. Nchi nyingi hususan za Ulimwengu wa Kiislamu zinapinga hatua za utawala wa Kizayuni na kutumia njia za diplomasia na michezo kuakisi malalamiko yao. Mwenendo huu unaonyesha wazi kuwa michezo pia inazidi kuhusishwa na masuala ya kisiasa.