Je, Tel Aviv inalenga kuizingira kimkakati Misri katika Bahari Nyekundu?
-
Je, Tel Aviv inalenga kuizingira kimkakati Misri katika Bahari Nyekundu?
Misri, katika kujibu kuongezeka kwa ushawishi na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Pembe ya Afrika, imeimarisha uwepo wake wa kijeshi nchini Somalia.
Kwa mujibu wa taarifa ya Pars Today, Misri, ikiwa inajibu kuongezeka kwa ushawishi wa Israel katika eneo, inaongeza uwepo wake wa kijeshi na kiusalama nchini Somalia na katika Pembe ya Afrika.
Baada ya hatua ya utawala wa Kizayuni kulitambua eneo lililojitenga la Somalia lijulikanalo kama Somaliland, hatua ambayo duru za kiusalama za Misri zinaiona kama tishio la moja kwa moja kwa uthabiti wa eneo na maslahi yake ya kimkakati, Cairo imeimarisha shughuli na ushiriki wake ndani ya Somalia.
Vyanzo vya kiusalama vya utawala wa Kizayuni vinasema kuwa Misri imeelekeza juhudi zake katika kuiunga mkono serikali ya Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Somalia, ili kulinda umoja wa eneo la Somalia na kuzuia athari zozote za kiusalama zinazoweza kujitokeza kutokana na shughuli za Tel Aviv katika Pembe ya Afrika.”
Maafisa wa Misri wanaamini kuwa hatua ya Israel kutambua Somaliland kama nchi huru ni sehemu ya juhudi pana zaidi za Tel Aviv kujijengea nafasi ya kimkakati karibu na Mlango wa Bahaari wa Bab al‑Mandeb na Bahari Nyekundu; eneo ambalo lina umuhimu wa kipekee kwa usalama wa baharini wa Misri.
Kwa mujibu wa wachambuzi, mvutano unaozidi kuongezeka kati ya Misri na utawala wa Kizayuni katika Pembe ya Afrika, hasa baada ya hatua ya Israel kutambua ‘Somaliland’, ni sehemu ya ushindani mpana zaidi wa kijiopolitiki ambao wahusika hawa wawili wanafuatilia katika ukanda wa Bahari Nyekundu, Bab al‑Mandeb na Afrika Mashariki.
Katika miaka ya karibuni, Pembe ya Afrika imegeuka kuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi ya ushindani kati ya nguvu za kikanda na zile za mbali, na mabadiliko yoyote katika mizani ya nguvu katika eneo hili yana athari za moja kwa moja kwa usalama wa taifa la Misri na maslahi ya kimkakati ya utawala wa Kizayuni.
Kwa miongo kadhaa, Misri imeitazama Pembe ya Afrika kama sehemu ya kina chake cha kimkakati. Usalama wa Bahari Nyekundu, udhibiti wa njia za biashara, na ulinzi wa Mfereji wa Suez ni masuala ya umuhimu wa juu kwa Cairo. Uwepo wa nguvu pinzani katika eneo hili, hasa katika pwani za Somalia, Djibouti au Eritrea, unaweza kuhatarisha usalama wa njia za baharini za Misri.
Kwa upande mwingine, utawala wa Kizayuni katika miaka ya karibuni umejitahidi kupanua mahusiano yake na nchi za Afrika ili kuongeza ushawishi wake katika eneo hili, na kulitumia kama chombo cha shinikizo dhidi ya Misri, Sudan na Yemen.
Kutambuliwa kwa Somaliland na utawala wa Kizayuni kunachukuliwa kuwa hatua muhimu katika mchuano huu wa kijiopolitiki. Somaliland ni eneo la kimkakati kaskazini mwa Somalia lenye mtazamo wa moja kwa moja juu ya Mlango Bahari wa Bab al‑Mandeb na njia muhimu za biashara ya kimataifa. Kwa hatua hii, Tel Aviv inalenga malengo kadhaa: kwanza, kujenga kituo cha ushawishi katika eneo linaloweza kuathiri usalama wa baharini wa Misri; pili, kupata mshirika mpya karibu na njia za usafirishaji wa nishati; na tatu, kuitumia Somaliland kama jukwaa la shughuli za kijasusi na kiusalama katika Afrika Mashariki, na hatimaye kama eneo la uwezekano wa kuwahamishia wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Misri inaiona hatua hii kuwa tishio la moja kwa moja dhidi ya usalama wake wa taifa. Cairo inahofia kwamba uwepo wa Israel katika Somaliland unaweza kusababisha kuanzishwa kwa vituo vya kijeshi au kijasusi karibu na njia za baharini, jambo ambalo linaweza kudhoofisha udhibiti wa Misri juu ya Bahari Nyekundu na hatimaye kuisukuma katika aina fulani ya kuzingirwa kimkakati na utawala wa Kizayuni.
Zaidi ya hayo, Misri tayari inakabiliwa na mgogoro wa Bwawa la Renaissance la Ethiopia, na ongezeko lolote la ushawishi wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Afrika Mashariki linaweza kubadilisha mizani ya nguvu kwa hasara ya Cairo, kwani Tel Aviv ina uhusiano wa karibu na Ethiopia na inaweza kuyatumia mahusiano hayo kuiwekea Misri shinikizo la moja kwa moja au lisilo la moja kwa moja.
Kwa upande mwingine, Misri katika miaka ya karibuni imejitahidi kuimarisha uhusiano wake na Somalia, Djibouti na Eritrea ili kuzuia kupenya kwa nguvu pinzani katika eneo hilo. Hatua ya utawala wa Kizayuni kuitambua Somaliland imeweka changamoto mpya kwa juhudi hizi na kuisukuma Cairo kuongeza uwepo wake katika ukanda huo. Ushindani huu umeongezeka hasa katika masuala ya usalama wa baharini, ushirikiano wa kijeshi, na uwekezaji katika bandari za eneo.
Athari za mvutano huu zinaweza kuwa pana. Kwanza, kuna uwezekano wa kuongezeka kwa mashindano ya kijeshi na kiusalama katika Pembe ya Afrika, eneo ambalo tayari limekuwa likikabiliwa na kutokuwa na utulivu, ugaidi na migogoro ya ndani. Jambo jingine ni kuongezeka kwa uwepo wa wahusika wa nje kama Marekani, China na Umoja wa Falme za Kiarabu katika eneo hili la kimkakati, hatua inayoweza kuongeza ugumu wa mazingira ya kisiasa na kiusalama, kwani kila moja ya nchi hizi inafuatilia maslahi yake maalum katika Pembe ya Afrika.
Dalili zinaonyesha kuwa hatua ya utawala wa Kizayuni kutambua Somaliland haikuwa tu mwendo wa kawaida wa kidiplomasia, bali sehemu ya mkakati mpana unaolenga kubadilisha mizani ya nguvu katika Afrika Mashariki na Bahari Nyekundu. Misri, ikitambua athari za hatua hii, imejitahidi kuimarisha uwepo wake katika eneo ili kuzuia kupanuka kwa ushawishi wa Israel. Mwelekeo huu unaashiria kwamba Pembe ya Afrika katika miaka ijayo itakuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi ya ushindani wa kijiopolitiki kati ya Cairo na Tel Aviv.