ECOWAS pia yatangaza kuiondolea vikwazo Guinea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136020-ecowas_pia_yatangaza_kuiondolea_vikwazo_guinea
Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imetangaza kuondoa vikwazo vyote vilivyobaki ilivyowekea Guinea kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Jan 29, 2026 06:05 UTC
  • ECOWAS pia yatangaza kuiondolea vikwazo Guinea

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imetangaza kuondoa vikwazo vyote vilivyobaki ilivyowekea Guinea kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.

Uamuzi wa Mamlaka ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo ulikuja baada ya mkutano wa kilele uliofanyika katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown jana Jumatano.

Jumuiya hiyo imebainisha kuwa, uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba 2025 nchini humo na kukabidhi madaraka kwa serikali iliyochaguliwa ya Rais Mamadi Doumbouya kisheria "kumeandaa mazingira faafu ya kurejeshwa kwa utawala wa kidemokrasia na heshima kwa utawala wa sheria nchini Guinea."

"Vikwazo vyote vilivyotangazwa dhidi ya Jamhuri ya Guinea katika muktadha wa kuwezesha kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba vimeondolewa," imesema taarifa hiyo, ambayo ilisainiwa na Julius Maada Bio, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo ambaye pia ni Rais wa Sierra Leone. Mwaka 2021, ECOWAS iliisimamishia Guinea uanachama na kuiwekea vikwazo kufuatia mapinduzi ya kijeshi.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Umoja wa Afrika kutangaza pia kuiondolea vikwazo Guinea ilivyoiwekea kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021, baada ya nchi hiyo kuandaa uchaguzi wa rais mwezi mwezi uliopita wa Disemba.

Aidha Umoja huo wa Afrika ulimpongeza kiongozi wa zamani wa jeshi, Mamady Doumbouya kwa kuchaguliwa kwake. Doumbouya aliapishwa karibuni kama rais mbele ya maelfu ya wafuasi wake na marais wa nchi kadhaa duniani.