Araghchi: Mazungumzo hayawezi kufanikiwa chini ya vitisho
-
Araghchi: Mazungumzo hayawezi kufanikiwa chini ya vitisho
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameonya kwamba, kutwisha diplomasia kupitia vitisho vya kijeshi hakuwezi kuwa na ufanisi au tija, akisema kwamba hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa na Tehran kufikia juu ya kufanya mazungumzo na Marekani.
Akizungumza na waandishi wa habari pambezoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri mjini Tehran jana Jumatano, Araghchi amesema hajafanya mawasiliano ya moja kwa moja katika siku za hivi karibuni na Mjumbe wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, Steve Witkoff, akisisitiza kwamba Iran haijawasilisha ombi lolote la kufanya mazungumzo.
Amebainisha kuwa, wapatanishi na nchi mbalimbali bado wanawasiliana na Iran, na kwamba Tehran inawasiliana na wadau hao waliochukua jukumu la kujenga nia njema. Hata hivyo, amesisitiza kwamba hakuna uamuzi wowote ambao umefikiwa kuhusu mazungumzo.
Akizungumzia maswali kuhusu wito wa mazungumzo kwa wakati mmoja na vitisho vya kijeshi vya Marekani mkabala wa Iran, Waziri Araghchi amesema kwamba 'vitisho na diplomasia' mara nyingi havitangamani katika mahusiano ya kimataifa.
Hata hivyo, amesisitiza kwamba msimamo wa Iran uko wazi: "Mazungumzo hayawezi kufanikiwa chini ya vitisho, na mazungumzo lazima yafanyike katika hali ambapo vitisho na kujitakia makuu kunawekwa kando."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameongeza kwamba, "Mazungumzo lazima yafanywe kwenye mazingira yenye mlingano, kwa kuzingatia heshima na maslahi ya pande zote mbili."
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amepinga utumiaji wa nguvu kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa, akisema mbinu kama hiyo haiwezi kutafsiriwa kama diplomasia.