Nujaba kwa maadui wa Iran: Vita vinaweza kufika milangoni kwenu
Katibu Mkuu wa kundi la kupambana na ugaidi la Harakat al-Nujaba la Iraq amewaonya vikali maadui wa Iran kuhusu matokeo mabaya ya uchokozi wowote mpya ambao wanaweza kufanya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mtandao wa al-Ahed wa Lebanon umemnukuu Sheikh Akram al-Ka’abi akisema hayo jana Jumatano na kueleza kwamba, uchokozi wowote mpya wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran utapanua wigo wa makabiliano katika eneo la Asia Magharibi, akisisitiza kwamba ikiwa vita vitaanza, upande utakaovianzisha hautaweza kuvimaliza.
Amesema shambulio kama hilo litawasha moto katika eneo zima la Asia Magharibi, na athari zake zinaweza kuenea zaidi ya medani ya vita. "Kisasi cha vita hivi kitapitishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kinaweza kufikia nchi na makazi ya wavamizi, bila mtu yeyote kuachwa," afisa huyo amesisitiza.
Al-Ka’abi amebainisha kuwa, shambulio kama hilo halitakosa kujibiwa, akiashiria uungaji mkono wa Iran kwa Iraq wakati wa makabiliano ya nchi hiyo ya Kiarabu dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), na kuongeza kwamba, watu wa Iraq hawatawasahau wale waliosimama nao katika nyakati ngumu.
Harakati ya Al-Nujaba ya Iraq imeyasema hayo kufuatia kuongezeka mvutano kati ya Iran na Marekani baada ya Rais Donald Trump kutishia kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Haya yanajiri siku chache baada ya Harakati ya Kata’ib Hizbullah ya Iraq (Brigedi za Hizbullah) kutangaza kuwa iko tayari kushiriki katika vita vyovyote vitakavyotokea ili kuilinda Iran, ikitoa wito kwa wanamapambano duniani kote kujiandaa kwa ajili ya hilo.