IRGC: Iran haitaanzisha vita, lakini ndiyo itakayoamua vitakavyoisha
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema Iran ndiyo inayoshikilia mpini na nafasi ya juu katika kuamua hatima ya vita vyovyote tarajiwa, likisisitiza kwamba kutumia mashinikizo ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu hakujazaa matunda.
Msemaji wa IRGC, Brigedia Jenerali Ali-Mohammad Naeini alisema hayo Jumatano, akiashiria uzoefu wa vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Israel na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu mwezi Juni ulionyesha kwamba, "chaguo la kijeshi dhidi ya Iran limeshindwa."
Afisa huyo pia amesema majaribio ya kuitisha Iran kupitia ishara na utumaji wa ndege za kivita, pamoja na meli ya kubeba ndege ya Marekani katika eneo, hayakuwa mapya, akielezea kama "mbinu ya zamani inayotumiwa na maafisa wa Marekani."
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya "kushindwa kwa haraka na kwa nguvu uasi unaoungwa mkono na Marekani nchini Iran," maafisa wa Marekani wamejaribu kuchochea mvutano na kueneza hofu ndani ya jamii ya Iran.
Wakati huo huo, Msemaji wa serikali ya Iran ameonya kwamba, ikibidi, jeshi la nchi hii litajibu mapigo ili kutetea mamlaka ya kujitawala na uhuru wa taifa, akitoa mfano wa kuingiliwa Iran waziwazi na wageni wakati wa ghasia za hivi karibuni.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Al Mayadeen ya Lebanon jana Jumatano, Fatemeh Mohajerani amesema Jamhuri ya Kiislamu inafadhilisha diplomasia, lakini haitavumilia majaribio ya maajinabi ya kuvuruga usalama wa nchi hii.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameonya kwamba, kutwisha diplomasia kupitia vitisho vya kijeshi hakuwezi kuwa na ufanisi au tija, akisema kwamba hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa na Tehran kufikia sasa juu ya kufanya mazungumzo na Marekani.