Ramaphosa: Hatutowarudisha Wapalestina waliokuja Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133196-ramaphosa_hatutowarudisha_wapalestina_waliokuja_afrika_kusini
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, makumi ya Wapalestina waliofika nchini humo kwa ndege ya kukodi hawatarudishwa bali watapewa hifadhi nchini Afrika Kusini.
(last modified 2025-11-15T05:22:01+00:00 )
Nov 15, 2025 05:22 UTC
  • Ramaphosa: Hatutowarudisha Wapalestina waliokuja Afrika Kusini

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, makumi ya Wapalestina waliofika nchini humo kwa ndege ya kukodi hawatarudishwa bali watapewa hifadhi nchini Afrika Kusini.

Rais Ramaphosa aliwaambia waandishi wa habari huko Soweto jana Ijumaa kwamba Wapalestina 153 waliotua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa O.R. Tambo juzi Alkhamisi wakiwa kwenye ndege ya kukodi wanashughulikiwa na mamlaka husika na hawatorudishwa walikotoka.

Ramaphosa amesema: "Jana tulikuwa na ndege iliyokuwa imewabeba Wapalestina 160 iliyotua O.R. Tambo na hawa ni watu kutoka Ghaza ambao kwa njia ya ajabu waliwekwa kwenye ndege iliyopitia Nairobi na kuja hapa na nilishapewa maelezo kuhusu suala hilo na Waziri wangu wa Mambo ya Ndani, akitaka kujua tunafanya nini kwa sasa, na nimesema hatuwezi kuwarudisha."

Ukosoaji mkubwa uliikumba serikali ya Afrika Kusini jana Ijumaa baada ya kuenea habari kwamba inawashikilia kwenye ndege kwa karibu saa 12 zaidi ya Wapalestina 150, akiwemo mwanamke ambaye ana mimba ya miezi tisa, kutokana na matatizo ya hati zao za kusafiria.

Mchungaji aliyeruhusiwa kukutana na abiria hao wakiwa bado wamekwama kwenye ndege alisema kulikuwa na joto kali na kwamba watoto walikuwa wakipiga kelele na kulia.

Abiria 153 wakiwemo watoto waliruhusiwa kutoka kwenye ndege Alkhamisi usiku baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini kuingilia kati na shirika lisilo la kiserikali linaloitwa Gift of the Givers kujitolea kuwahudumia.

Maafisa wa serikali ya Afrika Kusini wanaohusiaka na usimamizi wa mipaka wamesema kuwa, Wapalestina 23 wamesafiri hadi nchi zingine na kuwaacha 130 wakipewa nafasi ya kuingia nchini Afrika Kusini licha ya kutokuwa na vibali wala stakabadhi zozote zile.