Mashambulizi ya anga yaendelea Libya, 71 waokolewa baharini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133192-mashambulizi_ya_anga_yaendelea_libya_71_waokolewa_baharini
Mji wa Zawiya wa magharibi mwa Libya ulioko umbali wa kilomita 60 magharibi mwa mji mkuu Tripoli, umekumbwa na mashambulizi ya mfululizo ya anga. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya karibuni kabisa ya Shirika la Kudhibiti Vitisho vya Usalama mjini Zawiya.
(last modified 2025-11-15T05:21:14+00:00 )
Nov 15, 2025 05:21 UTC
  • Mashambulizi ya anga yaendelea Libya, 71 waokolewa baharini

Mji wa Zawiya wa magharibi mwa Libya ulioko umbali wa kilomita 60 magharibi mwa mji mkuu Tripoli, umekumbwa na mashambulizi ya mfululizo ya anga. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya karibuni kabisa ya Shirika la Kudhibiti Vitisho vya Usalama mjini Zawiya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulio hayo yamelenga boti kadhaa za doria za shirika hilo, ambazo zilikuwa na jukumu la kupambana na uvamizi wa baharini, mgendo ya binadamu na biashara haramu sambamba na kufanya shughuli za utafutaji na kuokoa wahamiaji haramu.

Katika taarifa hiyo, shirika hilo limelaani mashambulio ya anga yanayofanywa dhidi ya boti zake na kubainisha kuwa mashambulizi hayo ni mfano hatari na usio na msingi na yana athari za moja kwa moja kwa usalama wa taifa wa Libya.

Aidha limetaka kufanyika uchunguzi wa haraka na wa wazi ili kubaini wahusika na kuwawajibisha kikamilifu. Taarifa hiyo imetolewa baada ya mfululizo wa mashambulizi yaliyolenga boti na maeneo mbalimali ya bandari za Zuwara na Zawiya katika siku za hivi karibuni.

Huku hayo yakiripotiwa, wahamiaji sabini na mmoja wasio rasmi waliokolewa na Walinzi wa Pwani wa Jeshi la Taifa la Libya mashariki mwa nchi hiyo jana Ijumaa kutoka kwenye boti iliyopatikana umbali wa takriban maili 250 kaskazini magharibi mwa Benghazi.

Tovuti ya habari ya Al-Saa 24 imenukuu taarifa ya kikosi cha Walinzi wa Pwani ya Libya ikisema kuwa, kundi hilo lililookolewa linajumuisha raia 70 wa Bangladesh na mmoja wa Misri. Waliookolewa, baada ya kupokea msaada muhimu wa kimatibabu na kibinadamu, wamehamishiwa kwenye makazi maalumu ili kukamilisha taratibu za kawaida za kisheria.

Libya kwa muda mrefu imekuwa kitovu cha usafiri kwa wahamiaji haramu wanaojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya. Mazingira dhaifu ya usalama nchini humo tangu ilipoangushwa serikali ya Kanali Muammar Gaddafi mwaka wa 2011 yamechangia sana hali hiyo.