Jenerali Al Burhan hakutakuwa na suluhu baina ya SAF na RSF
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133190-jenerali_al_burhan_hakutakuwa_na_suluhu_baina_ya_saf_na_rsf
Mkuu wa jeshi la Sudan SAF Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan alisema jana Ijumaa kwamba hakutakuwa na "suluhu wala amani" kati ya jeshi analoongoza yeye SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF akisisitiza kwamba operesheni za kijeshi zitaendelea hadi "watakaposambaratishwa kabisa wanamgambo waasi."
(last modified 2025-11-15T05:20:47+00:00 )
Nov 15, 2025 05:20 UTC
  • Jenerali Al Burhan hakutakuwa na suluhu baina ya SAF na RSF

Mkuu wa jeshi la Sudan SAF Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan alisema jana Ijumaa kwamba hakutakuwa na "suluhu wala amani" kati ya jeshi analoongoza yeye SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF akisisitiza kwamba operesheni za kijeshi zitaendelea hadi "watakaposambaratishwa kabisa wanamgambo waasi."

Jenerali Al-Burhan, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mpito la Sudan, ametoa matamshi hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Al-Sreiha la Jimbo la Gezira katikati mwa Sudan. 

Amesisitiza kwamba, mgogoro wa Sudan hautotatuliwa kupitia makubaliano au kusitisha mapigano, akiapa kwamba mashambulizi dhidi ya RSF yataendelea hadi watakaposambaratisha kabisa RSF.

Pia amewataka Wasudan wote kushiriki katika kile alichokiita "vita vya utu na heshima," akitoa mwito kwa "yeyote anayeweza kubeba silaha" kujiunga na mapambano dhidi ya RSF.

Jenerali Al-Burhan amesisitiza pia kwamba watu wa Sudan hawatokubali kutawaliwa na RSF au wafuasi wake, akitoa mwito kwa jamii ya kimataifa kukusanya silaha kutoka kwa makundi hayo na kuleta amani ya kudumu nchini Sudan.

Tarehe 6 mwezi huu wa Novemba, RSF ilitangaza kukubali pendekezo lililowasilishwa na Kundi la Kimataifa la Quad la kutekeleza usitishaji mapigano kama sehemu ya hatua za awali za kufikia kusimamisha mapigano kwa malengo ya kibinadamu nchini Sudan.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyovuja, pendekezo hilo linalenga kuleta usitishaji mapigano kwa malengo ya kibinadamu kwa miezi mitatu ili kuruhusu kufikishwa misaada na baadaye kuingia kwenye mchakato wa kisiasa wa miezi tisa unaolenga kufikia suluhu kamili na ya kudumu ya kukomesha mapigano, lakini Mkuu wa Jeshi la Sudan SAF amepinga makubaliano yoyote ya amani na RSF.