Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu-4
(last modified Wed, 12 Mar 2025 09:28:14 GMT )
Mar 12, 2025 09:28 UTC
  • Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu-4

Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur´ani, kuwa mwongozo kwa watu, na hoja zilizowazi za uongofu na upambanuzi. Basi atayekuwa katika mji (wake) katika mwezi huu aufunge....

Tumo katika mwezi wa dhifa na ugeni wa Mwenyezi Mungu, mwezi ambao ni msimu wa machipuo wa ibada, na ndani yake milango ya rehma ya Mungu inafunguliwa kwa waja wake, na ni fursa ya pekee ya kurejea kwa Mola kwa toba na kuomba maghufira na msamaha kwake. 

Mwezi wa Ramadhani ni kama mji mtakatifu ambao kila mwaka huwa mwenyeji wa wageni wa Mungu kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja. Katika mwezi huu, kila kona ya mji inaishia kwa Mungu Mmoja, na historia yake inaanzia mwanzo wa uumbaji wa mwanadamu. Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu ndio wageni wa kwanza wa karamu hiyo adhimu, na Mungu Mwingi wa Rehma, Mwenye Ukuu usio na kifani, ndiye mwenyeji wa karamu na dhifa hiyo kubwa. Sisi pia ni mithili ya wapitanjia tunaotembea katika mitaa ya mji wa Ramadhani kwa matendo bora na amali njema. Tunapaswa kutumia vyema fursa hii ya mwezi wa karamu ya Allah kwa ajili ya kuhuisha agano letu na Mola Muumba. Kwa kawaida, mgeni anayekwenda ugenini kwa mkuu na mtu azizi na adhimu, hujipamba kwa mavazi yake maridadi na kujipaka uturu wenye harufu nzuri. Hivyo basi, katika safari yetu kwenye mji huo wa karamu ya Mola Muumba, tunapaswa kujipamba kwa vazi na taqwa na uchamungu, matendo mema na kutakasa zaidi nia zetu. Tukumbuke maneno ya Mtume Muhammad (saw) aliposema kabla kidogo ya kuanza mwezi wa Ramadhani kwamba: (Enyi watu)! Kwa hakika umekujieni Mwezi wa Allah kwa baraka, rehma na msamaha; Mwezi ambao ni bora zaidi ya miezi mingine mbele ya Mwenyezi Mungu, na siku zake ni bora kuliko siku nyingine. Nyusiku zake ni bora kuliko nyinginezo, saa zake ndizo bora kabisa kuliko saa zote. Ni mwezi ambao ndani yake mmekaribishwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu..   

makala yetu leo tunaipamba kwa Hadithi ya Mtume kipenzi na al Habib, Muhammad (saw) ambaye amesema:

: مَن صامَ للّه ِِ عَزَّ و جلَّ یوما فی شِدَّةِ الحَرِّ فَأصابَهُ ظَمَأٌ، وَکَّلَ اللّه ُ عَزَّ و جلَّ بهِ ألفَ مَلَکٍ یَمسَحُونَ وَجهَهُ و یُبَشِّرُونَهُ، حتّى إذا أفطَرَ قالَ اللّه ُ عَزَّ و جلَّ : ما أطیَبَ ریحَکَ و رَوحَکَ ! ملائکَتِی اشهَدُوا أنّی قد غَفَرتُ لَهُ .

 "Mwenye kufunga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakati wa joto kali la mchana na  kupatwa na kiu, Mwenyezi Mungu huwaamuru Malaika elfu moja wapanguse uso wake, na wampe bishara njema mpaka atakapofuturu. Kisha Mwenyezi Mungu husema: Ni nzuri iliyoje harufu na uturu wako. Enyi Malaika wangu! Shuhudieni kwamba mimi nimemsamehe."

Hadithii hii inatukumbusha kuwa, funga ya mwezi wa Ramadhani si kitendo cha kimwili tu, bali kinagusa undani wa nafsi ya mwanadamu na kumuweka karibu zaidi na Mungu, kiroho.

Kama tujuavyo, kufunga ni wajibu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, na Waislamu wote duniani hujizuia kula, kunywa na kadhalika katika mchana wa mwezi huu mtukufu. Katika mafundisho ya dini na Qur'ani Tukufu, funga imearifishwa kama mojawapo ya njia za kumkaribia M, Mungu SW. Kwa kufunga katika mwezi huu mtukufu, Waislamu hujishughulisha zaidi na ibada kuliko hapo awali, na kutakasa nafsi zao kwa kusoma Qur'ani, kuzidisha Swala na kuomba dua, sambamba na kustahamili kiu na njaa. Kufunga Swaumu kuna athari kubwa za kiroho. Mazoezi haya ya mwezi mzima hupunguza matamanio ya kidunia moyoni mwa mwanadamu na kumuelekeza kwenye ulimwengu wa kiroho na kimaanawi. Kufunga Swaumu pia hulainisha na kusafisha nafsi na kutayarisha moyo ili uwe tayari kupokea hakika za juu zaidi. Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwenye kufunga katika mwezi wa Ramadhani na akayazuia macho, masikio na viungo vyake vya mwili kufanya mambo yaliyoharamishwa, kusema uwongo na kusengenya, kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, Allah SW atamkurubisha kwake. 

Funga, kwa maana yake halisi, ina maana ya kutakasa nafsi na roho ya mwanadamu, na sio tu kuvumilia njaa na kiu. Imepokewa kwamba mwanamke mmoja alikuwa amefunga Swaumu, lakini alikuwa akimtukana na kumkera mara kwa mara jirani yake. Mtume aliposikia habari hiyo aliamuru mwanamke huyo atayarishiwe chakula (mchana wa Ramadhani). Mtume alimwambia yule mwanamke, kula chakula hiki. Yule mwanamke alijibu kwa mshangao: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nimefunga! Mtume alisema: "Unadai kuwa umefunga ilhali unamtukana jirani yako? Elewa kwamba, kufunga sio kuacha kula na kunywa tu. Mwenyezi Mungu ameifanya funga kuwa kizuizi dhidi ya maneno na mienendo mibaya." Kisha Mtume wa (saw) akasema kwa masikitiko na huzuni: “Ni wachache walioje waliofunga na wengi walioje walioshinda njaa."

Imepokewa pia katika kitabu cha Mizanul Hikma kwamba Mtume Muhammad (saw) alimwambia sahaba wake mwema, Jabir bin Abdillahil Ansari kwamba:

 یا جابر ! هذا شهر رمضان من صام نهاره وقام وردا من لیله وعف بطنه وفرجه وکف لسانه خرج من ذنوبه کخروجه من الشهر ، فقال جابر : یا رسول الله ! ما أحسن هذا الحدیث ، فقال رسول الله (صلى الله علیه وآله وسلم) یا جابر وما أشد هذه الشروط .

Ewe Jabir! Mwezi wa Ramadhani umeingia. Anayefunga mchana, akatumia sehemu yake ya usiku kwa ajili ya ibada, akazuia tumbo, utupu na ulimi wake kufanya haramu, atatoka katika madhambi yake kama atakavyotoka katika mwezi wa Ramadhani. 

Kisha Jabir alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni mazuri yaliyoje maneno haya! Mtume alisema: Na ni magumu yaliyoje masharti haya, Yaa Jabir?

Vilevile imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) katika Hadithi Qudsy kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Mtu ambaye viungo vyake havifungi na kujiepusha yale niliyoharamisha, sina haja ya yeye kuacha chakula na kinywaji chake kwa ajili yangu."

Mtume (saw) pia amesema, funga ya kweli ni ngao inayomkinga mwanadamu na Moto wa Jahannam: الصوم جنّة من النار

Mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Ja'far al Swadiq (as) pia amesema: “Ukifunga, hakikisha kwamba, masikio na macho yako yamefunga na kujizuia yaliyoharamishwa, na viungo vyote vya mwili wako vinajiepusha na maovu, na uache upuuzi na kumuudhi hadimu wako....     

Katika sehemu hii hebu tusikilize mojawapo ya dua zinazosomwa katika mwezi wa Ramadhani: 

اللَّهُمَّ قَوِّنِى فِیهِ عَلَى إِقَامَةِ أَمْرِکَ وَ أَذِقْنِى فِیهِ حَلاوَةَ ذِکْرِکَ وَ أَوْزِعْنِى فِیهِ لِأَدَاءِ شُکْرِکَ بِکَرَمِکَ وَ احْفَظْنِى فِیهِ بِحِفْظِکَ وَ سِتْرِکَ یَا أَبْصَرَ النَّاظِرِینَ: 

Ewe Mola wangu Mlezi! Nipe nguvu katika siku hii ya kutekeleza amri Zako. Na unionjeshe ndani yake utamu wa kukutaja Wewe. Na unifanikishe kukushukuru kwa ukarimu Wako. Na unilinde kwa ulinzi na sitara Yako. Ewe Mbora wa wenye kuona. ....

Dua hii inatukumbusha kuwa, mwanadamu anahitaji nguvu za kimwili na kiroho ili kuweza kumtumikia Mungu. Kwa hakika, kufunga ni mazoezi ambayo yanahitaji nguvu za kimwili na nguvu za roho, irada na azma thabiti ya mwanadamu. Tunapaswa kumuomba Allah atupe nguvu za kufanya ibada na kufunga katika mwezi huu wa Ramadhani.

Kumbukumbuka Mwenyezi Mungu na kutaja jina lake daima huipa nafsi furaha isiyo na kifani, kwa mtu ambaye amejaaliwa maarifa ya kumjua Allah SW. Mtu anayemjua Mungu ipasavyo humpenda, kumuashiki na kumkumbuka muda wote. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Yeyote anayependa kitu, basi kitu hicho huwa uradi katika ulimi wake. (مَن أحَبَّ شیئاً لَهِجَ بِذِکرِهِ؛) 

Mtu mwenye kufunga Saumu kama hii, dua yake inakubaliwa na kujibiwa na Mwenyezi Mungu, hasa wakati wa kufuturu. Hadhrat Imam Sadiq (as.) anahadithia kutoka kwa baba zake, kutoka kwa Amirul-Mu’minin (as), kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) kwamba amesema: 

اَربَعةٌ لاَ تُرَدُّ لَهُم دَعوةٌ وَتُفَتَّحُ لَهَا أَبوابُ السَّماءِ وَتَصِیرُ إلى العَرشِ : دُعاءُ الوَالِدِ لِوَلَدِهِ ، وَالمَظلومِ عَلى مَن ظَلَمَهُ ، وَالمُعتَمرِ حَتّى یَرجِعَ ، وَالصّائِمِ حَتّى یُفْطِرَ

Watu wanne dua zao hazikataliwi, na maombi yao hufunguliwa milango ya mbinguni na kufika kwenye Arshi: Dua ya mzazi kwa mtoto wake, dua ya mwenye kudhulumiwa dhidi ya aliyemdhulumu, dua ya mwenye kufanya Umra mpaka atakaporudi, na dua ya mwenye kufunga mpaka afungue Saumu yake.