Amir Saeed Iravani: Kamwe Iran haitasalimu amri mbele ya vitisho
-
Amir Saeed Iravani: Kamwe Iran haitasalimu amri mbele ya vitisho
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Tehran kamwe haitasalimu amri mbele ya vitisho vya kijeshi, mashinikizo ya kisiasa, au vikwazo vya kiuchumi.
Amir Saeed Iravani amelaani mashambulizi ya anga ya Israel ya Juni 2025 dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na kueleza hatua hiyo kama "kitendo cha uhalifu mkubwa" kilichotekelezwa saa chache baada ya azimio lililochochewa kisiasa la Bofi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Aliongeza kuwa mashambulizi hayo yameua na kujeruhi maelfu, yalilenga wanasayansi wa nyuklia na familia zao, na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye miundombinu muhimu.
Amelaani vikali Marekani na utawala wa Israel kwa mashambulizi haramu dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vinavyofanyika chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Aidha ameeleza kuwa, mashambulio ya Israel na Marekani dhidi ya Iran yalikiuka sheria za kimataifa, hatia ya Umoja wa Mataifa, kanuni za Wakala wa IAEA na azimio nambari 487 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameukosoa wakala wa IAEA na Mkurugenzi Mkuu wake kwa kushindwa kulaani mashambulizi hayo, licha ya taarifa za mara kwa mara za shirika hilo kwamba maeneo ya nyuklia hayapaswi kulengwa kutokana na hatari kubwa zinazoweza kusababisha usalama wa umma, mazingira, na usalama wa kimataifa. Amesema ukimya huo unadhoofisha uaminifu na mamlaka ya kimaadili ya wakala huo wa kimataifa wa nishati ya atomiki.