Afrika Kusini inafuatilia kesi ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Israel
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa tuhuma za kutenda mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa rasmi, Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini imesisitiza kuwa, tangazo la usitishaji vita halitafutilia mbali au kuficha jinai zilizotendwa wakati wa mashambulizi ya Israel, na kwamba kusitishwa kwa muda mapigano hakumaanishi kuhitimisha kesi ya ukiukaji sheria.
Wizara hiyo meeleza kuwa, madhumuni ya kuwasilisha kesi dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Mahakamani The Hague ni kuzuia kukariruwa uhalifu na kuhakikisha uwajibikaji kamili.
Afrika Kusini pia inaona njia hii ya kisheria kuwa inaendana na misimamo yake ya kihistoria katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na kuunga mkono mataifa yaliyokandamizwa.
Afrika Kusini iliwasilisha kesi hiyo Desemba 2023, ikiishutumu Israel kwa vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.
Mnamo Oktoba 2024, Afrika Kusini iliwasilisha mbele ya Mahakama ya Haki ICJ maelezo ya kina ya kurasa 500, huku hoja za utawala wa kizayuni za kupinga madai hayo zikitarajiwa kuwasilishwa Januari 12, 2026. Usikilizaji wa kesi unatarajiwa kufanyika mwaka 2027, na hukumu ya mwisho inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huo au mapema 2028.
Nchi kadhaa zimejiunga, au zimetangaza nia ya kufanya hivyo, katika kesi ya ICJ kuiunga mkono Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na Uhispania, Ireland, Uturuki na Colombia.