Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (3)
(last modified Wed, 12 Mar 2025 09:13:04 GMT )
Mar 12, 2025 09:13 UTC
  • Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (3)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza kipindi kingine maalumu ambacho tumekutayarishieni kwa mnasaba wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Huu ni mwezi ambao ni wa machipuo ya ibada, mwezi ambao milango ya rehema ya Mwenyezi Mungu huwa imefunguliwa kwa ajili ya kuwakaribisha waja wake na ni mwezi ambao huambatana na fursa chungu nzima kwa ajili ya kuwawezesha waja wake kurejea kwenye hakika ya dhati zao.

Mwezi wa Ramadhani ni fursa ya kuhuisha moyo wa kimaanai, na pia ni fursa ya kujitakasa na kujikarabati kidhati. Njooni tuungane pamoja kwa ajili ya kunufaika na baraka za mwezi huu uliojaa nuru na tuitikie mwaliko na dhifa ya Mwenyezi Mungu kwa kuomba dua na kufanya ibada kwa nia safi.

******

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Hijiria na ni mwezi bora na uliojaa fadhila zaidi kati ya miezi yote ya kalenda hiyo. Kwa kuwadia mwezi wenye nuru wa Ramadhani, Malaika hupaza sauti kwa kusema: "Ewe Mwanadamu! Elewa kwamba katika mwezi huu, milango yote ya Jahannam imefungwa, Shetani amefungwa pingu na milango ya Pepo imefunguliwa kwa ajili ya kuwakaribisha waja wa Mwenyezi Mungu. Hivyo Jitayarisheni kwa ajili ya kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu na kuingia kwenye Pepo kwa kufunga na kufanya ibada.

Watu walioghafilika hupuuza wito huo wa Mungu na hivyo kujinyima fursa ya kunufaika na rehema pamoja na msamaha wake. Ama waja walio na nyoyo safi zenye mwamko na ambao kwa hakika ni waumini halisi hutambua kwamba ni lazima wanufaike vya kutosha na fursa hii ya kipekee na kuchuma maua yenye harufu nzuri na ya kuvutia zaidi kutoka kwenye bustani hii.

Tunapasa kuingia na kunufaika vilivyo na mvua ya Ramadhani na hivyo kufaidika na msimu huu wa kuchanua na kuchipua kimaanawi maua na majani ya mimea katika kipindi hiki malumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi huu ni fursa isiyo na mfano wake kwa ajili ya waja ambao wanataka kujiweka mabli na mafungamano ya kidunia na kuweka nyoyo zao mbele ya upepo mwanana wa rehema ya Mwenyezi Mungu.

******

Katika dhati ya kila mwanadamu kuna nguvu na wito wa kiungu ambao, kama alivyo rafiki mwema na mwenye huruma, humuita na kumshawishi afanye mambo mema na kujitenga na ufisadi na maovu. Nguvu hii iko ndani ya dhati zetu na kufuata maagizo na makatazo yake kunachukuliwa kuwa ni ukamilifu na fadhila.

Nguvu hii ambayo hujulikana kama 'dhamiri', ni kizuizi muhimu ambacho kila mara tunapofanya kosa hutuzomea na kutufanya tujutie tulichokifanya. Jambo la kuvutia ni kwamba tunapofanya jambo jema, dhamiri hii husisimka na kuleta furaha ndani ya mioyo yetu.

Wito wa dhamiri daima hutukumbusha na kututaka turekebishe makosa na udhaifu wetu na wakati huo huo kututaka tufidie kasoro zinazotokana na dhambi. Qur'ani tukufu inauita wito huu wa ndani kwa jina la 'Nafs Lawwamah' kwa maana ya nafsi inayokemea au kulaumu.

Huenda umeshaona watu wengi ambao wamebadilisha maisha yao yaliyojaa uhalifu na dhambi chini ya ushawishi wa wito huu na kisha kufungua ukurasa mpya katika maisha yao. Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, wito huu wa dhamiri hufikia kilele chake ambapo wageni wa Mungu hutegemea nguvu hii ya ndani kwa ajili ya kuzidisha ibada, kuomba dua na kufarijika zaidi na Mola wao.

********

Moja ya malengo yanayovutia zaidi ya mafundisho ya dini ni kuifanya nguvu hii ya dhamiri iweze kuamka na kusisimuka ndani yetu siku zote. Swala, usomaji Qur'ani, hisani na kuwasaidia wengine ni kama maji safi yanayoimarisha nguvu hii ya ndani na kulea dhamiri ya juu na yenye nguvu zaidi inayoitwa "dhamiri ya kidini". Katika nyakati za majaribu ya shetani na fikra mbaya, dhamiri hii ya kidini, kama anavyofanya rafiki anayetujali, huamka mara moja kwa ajili ya kutunusuru na kutupa ufahamu na nguvu ya kuepuka dhambi inayohatarisha maisha yetu na hutuweka mbali nayo.

Funga ni ibada ambayo hutekelezwa kwa nia safi na kwa lengo la kufuata dhairi ya kidini. Hivyo ria, kujionyesha mbele ya watu na nia nyingine mbaya huonekana mara chache sana kwenye ibada hii tukufu. Funga ina maana ya kuwa na subra na kujizuia mambo kama vile kula na kunywa wakati wa mchana. Mtu anapofunga ibada yake huwa na thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Imam Ali (as) anasema kuwa mtu kama huyu huwa amefikia kiwango cha ukamilifu wa dhamiri ya kidini kwa sababu funga humfanya aweze kutambua majukumu yake na kumuongoza kweye mambo mema. Katika mwezi huu mtukufu, kwa kufunga na kuimarisha dhamiri yetu ya kidini tunaweza kutambua dhati zetu na hivyo kuchukua hatua zinazofaa kuelekea utendaji wa mambo mema na ya fadhila. Hii ni fursa ambayo hatupasi kuipoteza kwa ajili ya kujiimarisha kimaanawi.

*****

Tunasoma katika dua ya siku ya tatu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kama ifuatavyo: "Ewe Mwenyezi Mungu! Katika siku hii, niruzuku mwamko na niepushe na upumbavu, ujinga na mambo ya batili. Na tunufaishe pia na kila heri ambayo unaiteremsha katika siku hii, ewe Mkarimu wa Wakarimu."!

Watu wengi hudhani kuwa riziki huhusiana tu na mambo ya kimaada. Hii ni katika hali ambayo riziki hujumuisha neema zote za Mwenyezi Mungu, ziwe ni za kimaada au za kimaanwi. Moja ya neema bora zaidi za Mwenyezi Mungu ni elimu na kuwa na mwamko kinyume cha ujinga na kutokuwa na ufahamu. Ili kufanya vizuri mambo yake mwanadamu anahitajia uelewa na maarifa ambapo akili ndiyo rasilimali na chimbuko la uelewa huu. Mwanadamu hukamilika kwa kuwa na akili salama. Akili humuongoza kwenye njia nyoofu na ni ufunguo wa kila jambo. Akili hii hufanya kazi inavyotakiwa inapopata msaada na mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

****

Akili na hekima ni mtaji wa maisha na ibada ya mwanadamu, na busara ni mwanga wa njia ya wokovu. Akili iliyo mbali na kuchanganyikiwa, kasoro na vumbi la ujinga na ushirikina inaweza kuelewa vizuri zaidi ukweli na hakika ya mambo.

Bila shaka akili na busara kama yalivyo mambo mengine ni baraka ambayo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu. Kwa hiyo, tunamwomba aweze kutupa akili na mwamko wa kutosha ili tuweze kutekeleza vyema mambo yetu, hasa kuhusiana na maamrisho na makatazo yake.

Ujinga ni kinyume cha hekima. Tofauti na alivyo mtu mwenye hekima na busara anayefanya mambo kwa msingi wa sifa mbili hizo, tabia na matendo ya mtu mjinga hayana mantiki. Mtu mnafiki na mwenye ria hujaribu kujionyesha kuwa mbora kuliko alivyo na hivyo kuficha ukweli wa dhati yake. Katika dua hii, Tunamwomba Mwenyezi Mungu asitujaalie kuwa miongoni mwa watu wapumbavu na wadanganyifu.

*****

Wapendwa wasikilizaji, tumefikia mwisho wa kipindi cha tatu cha "Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu". Tunatumai kipindi hiki kimekuhimiza vya kutosha ili nawe upate kunufaika na baraka za mwezi huu mtukufu. Katika kipindi kinachokuja, tutajadili sehemu nyingine ya fadhila nyingi zinazopatikana katika mwezi huu mtukufu. Basi hadi wakati huo, jaribu kuwa karibu zaidi na Mweneyezi Mungu kwa kuomba na kutumia vizuri fursa za mwezi huu mtukufu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.