Araghchi azijia juu nchi zinazotetea uchokozi wa Israel, US dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128568-araghchi_azijia_juu_nchi_zinazotetea_uchokozi_wa_israel_us_dhidi_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema kuwa, hujuma za Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na haki za binadamu za kimataifa, akikosoa misimamo ya upendeleo ya baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuhalalisha vitendo hivyo vya uchokozi vilivyofanywa na utawala wa Israel na Marekani mwezi uliopita.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jul 21, 2025 01:57 UTC
  • Araghchi azijia juu nchi zinazotetea uchokozi wa Israel, US dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema kuwa, hujuma za Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na haki za binadamu za kimataifa, akikosoa misimamo ya upendeleo ya baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuhalalisha vitendo hivyo vya uchokozi vilivyofanywa na utawala wa Israel na Marekani mwezi uliopita.

Katika mazungumzo ya simu na Ignazio Cassis, Mkuu wa Idara ya Mashauri ya Kigeni ya Uswisi, Sayyid Araghchi amesisitiza haja ya nchi zote kuchukua msimamo thabiti kulaani ukiukaji huu wa wazi wa sheria za kimataifa na kuwawajibisha wahusika.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameonya kwamba, misimamo ya upendeleo ya baadhi ya nchi za Ulaya katika kuhalalisha uchokozi huo inaweza kushajiisha na kuufanya kuwa kawaida uvunjaji wa sheria.

Sayyid Abbas Araghchi ameeleza bayana kuwa, kuendekeza mienendo hiyo hakutakuwa na matokeo mengine ghairi ya kukithiri ukosefu wa usalama kieneo na kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Uswisi amethibitisha tena uungaji mkono wa nchi yake kwa diplomasia na akaelezea utayarifu wa kushirikiana katika suala hili. Vile vile ametaja mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kuwa ni kinyume na kanuni za kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na juhudi za kuzuia kuongezeka kwa mivutano na ukosefu wa usalama katika eneo.

Mnamo tarehe 13 Juni, utawala haramu wa Israel ulifanya shambulizi dhidi ya Iran bila sababu, likiwalenga makamanda wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia wa nchi hii.

Mashambulizi hayo kwenye maeneo ya makazi pia yalisababisha vifo vya mamia ya raia, jambo ambalo liliifanya Iran kutoa majibu madhubuti. Hata hivyo, mzozo huo ulikoma mnamo Juni 24 wakati utawala wa Kizayuni ulipoomba kusitishwa kwa mapigano kufuatia wimbi la mashambulizi ya makombora ya kulipiza kisasi ya Iran.