Hamas: Netanyahu hana nia ya kufikia makubaliano ya usitishaji vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128346-hamas_netanyahu_hana_nia_ya_kufikia_makubaliano_ya_usitishaji_vita
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imesema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu hana azma kabisa ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, ili kuhitimisha kampeni ya mauaji ya halaiki inayoendelea katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jul 15, 2025 01:22 UTC
  • Hamas: Netanyahu hana nia ya kufikia makubaliano ya usitishaji vita

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imesema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu hana azma kabisa ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, ili kuhitimisha kampeni ya mauaji ya halaiki inayoendelea katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina ilisema kwamba, "mhalifu Netanyahu" analitumbukiza jeshi lake na utawala wake katika vita visivyo na maana wala matarajio yoyote.

"Netanyahu ana ujuzi wa kusambaratisha duru moja ya mazungumzo baada ya nyingine, na hataki kufikia makubaliano yoyote," Hamas imesema.

Kundi hilo la wanamuqawama limeeleza bayana kuwa, "ushindi kamili" ambao Netanyahu anausaka kwa udi na uvumba ni njozi kubwa inayokusudia kuficha kushindwa kwake katika medani ya vita [huko Gaza] na katika siasa.

Haya yanajiri huku vikosi vya Israel vikiendelea kumwaga damu za Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza, mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa.

Katika mashambulizi ya jana Jumatatu, wanajeshi makatili wa Kizayuni waliua shahidi Wapalestina 78 wakiwemo kadhaa waliokuwa wanatafuta misaada ya kibinadamu huko Gaza, huku kukiwa na ongezeko la mgogoro wa mafuta na njaa.

Mashambulizi hayo yanaripotiwa huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiendelea kuomba msaada zaidi kuruhusiwa kuingia Gaza, ambako baa la njaa linalikabili eneo hilo, huku uhaba mkubwa wa fueli ukiipigisha magoti sekta iliyodhoofika ya afya.