Madai ya madola ya Ulaya kuhusu kutaka amani sambamba na kuunga mkono jinai za Israel
Jibu halali la kijeshi la Iran dhidi ya vitendo vya kigaidi na kichokozi vya utawala ghasibu wa Israel liyafanya mataifa ya Ulaya kuhaha na sasa yanadai kuwa ni wapigania amani.
Bila shaka ni kioja na kichekesho kwa madola ya Ulaya kudai kutaka amani katika hali ambayo yanaunga mkono kwa hali na amali jinai za utawala ghasibu wa Israel huko Palestina na Lebanon. Katika radiamali ya hatua za kujihami za Hizbullah ya Lebanon na jibu la Iran kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametoa ahadi kusitishwa mashambulizi dhidi ya Israel kwa kushirikiana na washirika wa Israel ili kupatikane usitishaji vita kati ya Israel na Hizbullah ya Lebanon. Watu wa Ulaya hususan madola makubwa ya bara hilo kama Ujerumani, hayajawahi kuwa wapatanishi waaminifu na wasioegemea upande wowote katika uvamizi wa Wazayuni wanaoikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina.
Sera hii haikomei kwa matukio ya baada ya tarehe 7 Oktoba mwaka jana tu na uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Gaza. Tangu kutangazwa kuasisiwa utawala bandia wa Israel huko Palestina mwaka 1948, madola ya Ulaya daima yamekuwa yakiwatetea na kuwakingia kifua Wazayuni. Wazayuni wanaoikalia kwa mabavu Palestina nao wakitegemea uungaji mkono huu hawajaacha kufanya jinai yoyote. Baada ya operesheni ya kimbunga ya Al-Aqswa, viongozi wengi wa tawala za Ulaya, akiwemo Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, walifika Tel Aviv na kutangaza uungaji mkono wao kamili kwa Israel. Bila kuashiria hata kidogo jinai za Wazayuni, viongozi hao walikuwa wakiitaka Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kuwaachia huru mateka wa Israel bila ya masharti yoyote.

Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa na watetezi wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi, hakuna jinai ambayo haijafanywa na Wazayuni huko Gaza. Mtazamo wa kujiona bora na wa ubaguzi wa viongozi wa utawala wa Kizayuni umekwenda mbali zaidi na kufikia hatua ya kumkosoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa kutolaani shambulio la Iran dhidi ya Israel ambalo kimsingi limetekelezwa katika fremu ya haki ya kujihami ya Iran kwa mamlaka yake na umoja wa ardhi yake.
Kutokana na Guterres kutolaani shambulio hilo la makombora la Iran dhidi ya Israel, Wazayuni wametangaza kumpiga marufuku Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kuingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Mtazamo huu kujiona bora na wa kibaguzi wa Wazayuni pia unashuhudiwa miongoni mwa tawala za Magharibi. Tawala za Magharibi zinajiona kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani.
Vigezo vya tawala za Ulaya katika kutoa fasili na maana ya haki za binadamu vinaweza kutathminiwa katika radiamali na majibu yao kwa jinai ya Wazayuni na utetezi halali wa Wapalestina katika ardhi ya mababu zao na kukabiliana na uchokozi wa Wazayuni. Madola ya Ulaya yanazitambua harakati za muqawama za Palestina na Lebanon kuwa ni magaidi kwa sababu ya kusimama kwao kidete dhidi ya hujuma za Wazayuni, lakini yanazichukulia hujuma za Wazayuni na mauaji ya makumi ya maelfu ya watu huko Palestina na Lebanon kuwa eti ni haki halali ya kujilinda na hata kuunga mkono hilo.

Vipi watu wanaotetea ardhi zao na kujihami mbele ya uvamizi wanaonekana kuwa ni magaidi, lakini wale wanaovamia ardhi ambayo si yao na wanafanya mauaji kila leo wanaonekana kuwa ni wenye kujitetea na kujihami na kwamba, wana haki ya kufanya hivyo? Je, sera hii kama sio kujiona bora na kufanya ubaguzi ina maana gani? Madola ya Magharibi hupaza sauti za kupigia debe suala la haki za binadamu pale anapouawa Myahuidi mmoja mlowezi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, lakini hawaonyeshi hata kusikitishwa tu na mauaji ya kila siku ya makumi ya maelfu ya wanawake na watoto wa Kipalestina na Lebanon. Ni haki gani za binadamu zinazozungumziwa na madola ya Ulaya?
Mtazamo huu wa kinafiki na kindumakuwili ulishuhudiwa bayana pia saa chache tu baada ya hatua halali ya Iran na kurusha makumi ya makombora ya balestiki na kulenga vituo kadhaa vya kijeshi vya Israel na vituo vya kijasusi. Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von Derlein alitoa taarifa akisema: "Ninalaani vikali shambulizi la makombora ya balestiki la Iran dhidi ya Israel. Vitendo kama hivi vinahatarisha uthabiti na amani ya kikanda na wakati huo huo vinapanua wigo mivutano katika hali isiyokuwa na utulivu."

Cha ajabu ni kwamba, maafisa na viongozi hawa hawa wa Ulaya wanaoonyesha kuwa na wasiwasi na amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi hawakuonyesha hisia zozote wakati ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria uliposhambuliwa na Wazayuni na washauri kadhaa wa kijeshi wa Iran walipouawa shahidi, au alipouawa shahidi Ismail Haniyeh ndani ya ardhi ya Iran. Lakini wanaona hatua ya Iran ya kujihami na kulinda mamlaka yake ya kujitawala ambayo ni hatua halali kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa kuwa inahatarisha amani na usalama wa eneo.
Mtazamo huu wa kindumakuwili, kinafiki, wa kujiona bora na wa kibaguzi wa madola ya Ulaya hauna natija zaidi ya moja nayo ni kuchochea ukosefu wa amani na usalama wa Asia Magharibi kwa kuwaunga mkono Wazayuni maghasibu na wavamizi. Kwa kuendesha siasa hizi za kindumakuwili tawala za Ulaya zimethibitisha kwamba, madai yao ya kutaka na kupigania amani ni urongo mtupu na kimsingi ni washirika wa jinai zote za Israel huko Palestina na Lebanon.