Iran inachunguza ombi la Marekani kuhusu kuanza tena mazungumzo ya nyuklia
(last modified Sat, 12 Jul 2025 07:08:32 GMT )
Jul 12, 2025 07:08 UTC
  • Iran inachunguza ombi la Marekani kuhusu kuanza tena mazungumzo ya nyuklia

Mshauri mwandamizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, amethibitisha kuwa Iran imepokea ombi kutoka Marekani kuhusu kuanza tena mazungumzo ya nyuklia, na amesema kwa sasa Tehran inachunguza pendekezo hilo kwa kina.

“Baada ya vita vya Israeli-Marekani, hatuiamini kabisa Marekani,” amesema Ali Larijani katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera.

Utawala wa Israeli ulianzisha shambulio la wazi na la kichokozi dhidi ya Iran tarehe 13 Juni, ambalo liliambatana na ugaidi wa mauaji ya makamanda wakuu wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia pamoja na raia.

Tarehe 22 Juni, Marekani nayo ilijiunga rasmi na vita dhidi ya Iran kwa kutekeleza mashambulizi kwenye vituo vitatu vya nyuklia nchini humu, jambo ambalo ni ukiukaji wa Hati ya Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Kutokomeza Silaha za Nyuklia.

Mashambulio ya Israel yalitokea wakati Iran na Marekani zilikuwa zimefanya raundi tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, yaliyoendeshwa na Oman, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran tangu mwezi Aprili na zilikuwa zinajiandaa kuanza mazungumzo mapya mjini Muscat tarehe 15 Juni, ambayo yalifutiliwa mbali.

Larijani amebainisha kuwa, “Nadharia ya Marekani, inayoongozwa na Rais Donald Trump, inategemea kanuni ya kwamba ima usalimu amri au ukabiliwe na vita.”

Ameongeza kwamba “Mashariki ya Kati mpya” inaibuka, ambayo itakuwa ni eneo lenye uthabiti na huru.

Katika tukio tofauti, Larijani alisema Ijumaa kwamba rais wa Marekani na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wanafuata nadharia ya  “amani kupitia mabavu” na kuongeza kuwa, “huu ni mtazamo uleule ambao watu wote wenye tamaa ya kufyonza damu katika historia wamekuwa nao, na si jambo jipya.”

Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu alikuwa akizungumza wakati wa Khitma ya shahidi Brigedia Jenerali Mohammad Saeed Izadi, anayejulikana kama Haj Ramezani,  aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Palestina cha Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Kifo cha Jenerali Izadi kilithibitishwa na IRGC mwishoni mwa Juni, siku chache baada ya kujeruhiwa vibaya katika shambulio la Israel.

Larijani alisema Marekani imesababisha uharibifu na mauaji makubwa katika ulingo wa kimataifa, lakini watu wa Palestina na Gaza hawakukubali kusalimu amri.

Ameongeza kuwa, “Iran, chini ya uongozi wenye busara wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ilijibu kwa nguvu na haikuruhusu nadharia hii kutekelezwa nchini Iran. Kwa hiyo, nadharia ya Trump imefeli.”