Araghchi: Iran haijasitisha ushirikiano wake na IAEA
(last modified Sat, 12 Jul 2025 14:29:20 GMT )
Jul 12, 2025 14:29 UTC
  • Araghchi: Iran haijasitisha ushirikiano wake na IAEA

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, ushirikiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haujasimamishwa na kusisitiza kuwa, sisitizo la Ulaya kuhusu kuhuisha mchakato wa kurejeshwa vikwazo vya nyuklia dhidi ya Tehran litahitimisha jukumu lao katika faili la atomiki la Jamhuri ya Kiislamu.

Sayyid Abbas Araghchi ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mkutano na mabalozi, mabalozi wadogo, na wakuu wa misheni za kigeni hapa mjini Tehran katika uwanja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo Jumamosi.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inazishukuru nchi zote zilizolaani hujuma za hivi karibuni za Israel dhidi ya Iran na kusema kuwa, "Takriban nchi 120 zililaani hujuma za utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Iran."

Sayyid Araghchi amesisitiza kwamba, ushirikiano na IAEA haujakoma na kuongeza kuwa "Iran imekuwa mwanachama mtiifu wa NPT na imeshirikiana na shirika hilo." "Ushirikiano wetu na wakala huo haujakoma, ndio kwanza umepata muundo mpya. Kuanzia sasa, uhusiano na Wakala utasimamiwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa (SNSC)."

"Ombi la wakala (wa IAEA) la kuendeleza ushirikiano na Iran litapitiwa upya kwa msingi wa kesi baada ya kesi na SNSC, na maamuzi yatafanywa kwa kuzingatia ulinzi na usalama," Waziri Araghchi ameeleza na kubainisha kuwa, "Ukweli wa mambo ni kwamba, vifaa vyetu vya nyuklia vilishambuliwa na kwamba kukaribia vituo hivi kwa sasa ni hatari, ikiwa ni pamoja na kuenea kwa vifaa vya mionzi au mripuko, na tunadhani, suala la ulinzi na usalama ni suala la wasiwasi kwa wakaguzi wanapokaribia vituo hivi."

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa "Hakuna njia nyingine isipokuwa kurejea kwenye diplomasia." "Hakuna njia nyingine ila kurejelea diplomasia na suluhu iliyojadiliwa na iliyokubaliwa, na vita vya hivi majuzi vilithibitisha hili hata zaidi kuliko hapo awali."