Baadhi ya Waislamu Kenya wapendekeza Kadhi Mkuu ajaye atoke nje ya Pwani
Baada ya kupita siku chache tu tangu alipoaga dunia Kadhi Mkuu wa Kenye Sheikh Abdulhalim Hussein Athman, baadhi ya Waislamu wamependekeza kadhi ajaye atoke nje ya eneo la Pwani.
Naibu Kadhi Mkuu Sukhyan Hassan amekiri kuwa kuna msukumo unaotolewa wa kutaka wadhifa huo uende nje ya Pwani lakini akasema suala hilo liko mikononi mwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) ambayo ndiyo mwaajiri.
“Sheria inasema kuwa kunastahili kuwe na tangazo, mahojiano na mtu bora zaidi ateuliwe kadhi mkuu. Hata hivyo, baadhi wanauliza nafasi ya naibu kadhii mkuu ina maana gani kama hawezi kurithi nafasi hiyo jinsi ilivyo kwenye asasi nyingine za serikal,” amesema Bw Hassan anayetoka kaskazini mashariki kwenye mahojiano na Taifa Leo.
“Wadhifa huo haujetengewa eneo moja pekee ila maswali yameibuliwa iwapo kadhi mkuu atakuwa anatoka eneo moja tu, japo mwenyewe sitaki kujiingiza katika suala hilo,” akaongeza akisema kuna mahakama ya kadhi maeneo mengine nchini na si Pwani pekee.
Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Nchini (SUPKEM) Hassan Ole Naado yeye amesema Katiba ya 2010 i wazi kuhusu uteuzi na mchakato wa urithi wa kadhi mkuu.
“Mwaajiri ni JSC na iwapo yeyote anahisi amefuzu basi atume maombi wadhifa huo ukitangazwa na wakiwa bora wataupata. Hata Sheikh Abdulhalim alipata wadhifa huo baada ya mchakato unaoeleweka kufuatwa,” amesema Bw Naado.
Imam wa Msikiti wa Mumias Sheikh Abbas Abdulaziz naye alipendekeza kadhi mkuu atoke nje ya Pwani kwa sababu kuna dhana kuwa wasiotoka huko hawathaminiwi kama Waislamu wa kweli.
“Kuna dhana wenye rangi fulani ndio wanajua dini kuliko sisi lakini hilo si kweli. Kwa hivyo, kuwa na kadhi mkuu kutoka nje ya Pwani itakuwa afadhali na itazima mianya hiyo ya migawanyiko,” akasema Sheikh Abdulaziz ambaye pia ni mwenyekiti wa Supkem tawi la Mumias.
Aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Kenye Al Marhum Sheikh Abdulhalim Hussein Athman alifariki dunia siku usiku wa manane wa kuamkia Alkhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 55 na kuzikwa siku hiyohiyo.
Aliteuliwa kuwa Kadhi Mkuu Julai 17, 2023, na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), kuhchukua nafasi iliyoachwa wazi na Sheikh Ahmed Muhdhar aliyestaafu Disemba 2022 na kuwa Kadhi Mkuu wa 12 nchini Kenya.../